Kaunti zatakiwa kutumia chanjo zote za Covid-19

Muhtasari

• Waziri wa Afya Mutahi Kagwe siku ya Alhamisi alisema huenda baadhi ya kaunti zinashikilia chanjo za AstraZeneca ili kuzitumia kwa awamu ya pili ya chanjo.

Serikali za kaunti zimetakiwa kutumia chanjo zote za Corona katika hifadhi yazo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe siku ya Alhamisi alisema huenda baadhi ya kaunti zinashikilia chanjo za AstraZeneca ili kuzitumia kwa awamu ya pili ya chanjo.

Kagwe aliwahakikishia wadau na wananchi kwa jumla kuwa serikali bila shaka itafanikiwa kupata chanjo zingine ili kutekeleza awamu ya pili ya chacho.

Waziri anasema shirika la Covax limetoa hakikisho kwamba watapata awamu ya pili ya chanjo ya AstraZeneca.

Kumezuka hofu kuwa huenda wakenya waliopokea awamu ya kwanza ya chanjo ya AstraZeneca wakakosa kupata chanjo ya awamu ya pili baada ya serikali ya India kusitisha uuzaji wa chanjo ya AstraZeneca nje ya nchi hiyo kutokana na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Wizara ya afya ilikuwa tayari imekiri kuwepo ugumu kupata awamu ya pili ya chanjo ya AstraZeneca. Hali hii ililazimisha wizara ya afya kuongeza muda wa watu waliokuwa wamepata awamu ya kwanza ya chanjo kupata ya chanjo ya pili hadi wiki 12 kutoka wiki nane.

Kulingana na takwimu za hivi punde kiwango cha mambukizi kimeanza kushuka nchini Kenya, siku ya Alhamisi watu 495 walipatikana na virusi vya corona kutokana na sampuli 4,929 zilizopimwa chini ya saa 24.

Kati ya maambukizi hayo mapya 482 ni raia wa kenya ilhali 13 ni raia wa kigeni, 297 ni wanaume huku 198 wakiwa wa kike.

Kufikia sasa idadi ya jumla ya waliothibitishwa kuwa na corona imetimia 158,821.

Makali ya corona sasa yamefikia asilimia ya 10.0 huku jumla ya sampuli zilizopimwa zikitimia 1,664,435.

Watu 19 walipoteza maisha kutokana na corona na kufikisha idadi ya jumla ya 2,707 ya watu walioaga dunia kutokana na Covid-19 nchini Kenya..

Vile vile watu 242 walipona na kufikisha idadi ya jumla ya watu 108,124 waliopona. Watu 191 walipona wakiwa nyumbani huku 51 wakiruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali mbali mbali nchini.