Tanzia! aliyekuwa mbunge wa kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga afariki

Muhtasari

• Amekuwa akiugua kwa wiki mbili zilizopita katika Hospitali ya Reliance mtaani South C Nairobi.

• Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambi rambi kwa familia, marafiki na jamaa wa mbunge huyo wa zamani.

Mwakilishi wa zamani wa Wanawake katika kaunti ya Kwale Zainab Kalekye Chidzuga.

ameaga dunia.

Kifo cha mwanasiasa huyo kimethibitishwa na familia na marafiki wake wa karibu.

Amekuwa akiugua kwa wiki mbili zilizopita katika Hospitali ya Reliance mtaani South C Nairobi.

Mbunge huyo wa zamani aliyekuwa na umri wa miaka 65 anasemekana kuugua kutokana na athari za virusi vya Covid-19, kulingana na jamaa wa karibu.

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambi rambi kwa familia, marafiki na jamaa wa mbunge huyo wa zamani wa Kaunti ya Kwale.

Chidzuga, mtetezi mkuu wa utawala wa Jubilee na afisa wa zamani wa muda mrefu wa Shirika la Maendeleo Ya Wanawake (MYWO), alifariki siku ya Alhamisi.

Katika ujumbe wake, Rais alimsifia Chidzuga kama kiongozi thabiti na mhamasishaji mahiri wa msingi ambaye alisaidia kuinua ustawi wa wanawake katika Kaunti ya Kwale na kote nchini kupitia mipango yake mingi.

Rais aliitakia familia yake ujasiri na faraja ya Mungu wakati wanaomboleza.