Mmoja apigwa risasi katika mkutano wa F-Kenya Nairobi

Muhtasari

• Awali, mrengo wa Ford Kenya unaoongozwa na Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu ulitangaza kusimamisha mkutano wao kufuatia agizo la Mahakama ya kutatua mizozo ya vyama vya Kisiasa. 

• Eseli alikuwa amepanga kufanya mkutano wake Jumamosi lakini akabadilisha tarehe katika kile kilichoonekana kama mpango wa kukabiliana na Wetang'ula. 

Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula.
Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula.
Image: MAKTABA

Mtu mmoja alipigwa risasi wakati wa mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa chama cha Ford Kenya katika ukumbi wa Bomas of Kenya siku ya Alhamisi. 

OCPD wa Langata Benjamin Mwanthi alithibitisha mshukiwa alikamatwa. Mkutano wa wajumbe wa kitaifa wa chama hicho uliitishwa na mrengo wa chama hicho unaoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula. 

Awali, mrengo wa Ford Kenya unaoongozwa na Mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu ulitangaza kusimamisha mkutano wao kufuatia agizo la Mahakama ya kutatua mizozo ya vyama vya Kisiasa. 

Mahakama hiyo ilisimamisha mikutano hiyo miwili iliyokuwa ifanyike sambamba, mmoja uliitishwa na mrengo unaoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula na mwingine mrengo wa Eseli. Akizungumza katika mkao na wanahabari kilichofanyika katika hoteli moja ya Nairobi siku ya Alhamisi, Eseli alisema agizo hilo lilitolewa kielektroniki mnamo Jumatano saa kumi jioni. 

"Maandalizi ya mkutano wetu zilikuwa katika awamu ya mwisho. Tulikuwa tayari tumekodisha na hata kulipia ukumbi. Ingawa tumesikitishwa na uamuzi huo, tutatii maagizo kama tulivyofanya awali," alisema. 

Ugomvi kati ya pande hizo mbili ulikuwa umetishia kusambaratisha mipango ya kisiasa ya kiongozi wa chama Wetangu'la ambaye alikuwa katika hatari ya kupinduliwa. 

Viongozi wa mrengo wa pili wa Fork Kenya Wafula Wamunyinyi (kulia) Eseli Simiyu
Viongozi wa mrengo wa pili wa Fork Kenya Wafula Wamunyinyi (kulia) Eseli Simiyu

Eseli alikuwa amepanga kufanya mkutano wake Jumamosi lakini akabadilisha tarehe katika kile kilichoonekana kama mpango wa kukabiliana na Wetang'ula. 

Katika mkutano wa Wetang'ula, ajenda ilikuwa kuridhia sera na kanuni za chama, kufanyia marekebisho katiba ya chama, kuchagua maafisa wa kitaifa na kuteua mgombeaji wa urais wa chama. Wetang'ula alikuwa amefutilia mbali mkutano huo wa mrengo wa Eseli, akisema mbunge huyo wa Tongaren amezuiwa na mahakama kufanya shughuli zozote za chama.

“Wajumbe wote halali wa Ford Kenya kote nchini wamepokea mwaliko huo na wako tayari kuja, tunataka kuwahakikishia kuwa chama kiko imara na kimeungana na kwamba kuna NDC moja tu mnamo Novemba 4. Ninawahakikishia kuwa chama kiko imara na kimeungana,” alisema. 

Migogoro katika Ford Kenya ilianza Mei 2020 baada ya baadhi ya viongozi wake kuamua kumfukuza Wetang'ula kwa misingi ya utovu wa nidhamu.