Musalia Mudavadi kutohudhuria kongamano la Azimio la Umoja Ijumaa

Muhtasari
  • Musalia Mudavadi kutohudhuria kongamano la Azimio la Umoja Ijumaa
KInara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi
Image: Andrew Kasuku

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi ametoa taarifa kwamba hatahudhuria kongamano la Azimio la Umoja linalotarajiwa kuandaliwa katika ukumbi wa Kasarani hapo kesho.

Kwenye taarifa yake Mudavadi anasema kuwa atakuwa anashughulikia masuala ya kibinafsi na hivyo basi hataweza kufika kwenye kongamano hilo linaloandaliwa na chama cha ODM.

Mudavadi pia amesema kuwa mwaliko alioupokea ulikuwa wa kibinafsi kama kiongozi wa chama cha ANC na wala sio kama mmoja wa vigogo wa One Kenya Alliance.

Hata hivyo, amemtakia mema kinara wa chama cha chungwa Raila Odinga na kusema kuwa ni mmoja wa wapinzani wake kwenye kinyang’anyiro cha ikulu na hivyo basi anamuombea mema kwenye siku yake kuu hiyo kesho.

"Nimepokea mwaliko rasmi wa Kuhudhuria Mkutano wa Azimio la Umoja.

Kama ilivyobainishwa hapa, mwaliko huo ulishughulikiwa kwa nafasi yangu binafsi kama Kiongozi wa Chama cha ANC na sio Mkuu wa OKA.

Kwa kusikitisha, sitaweza kuhudhuria kwa sababu ya shughuli za kibinafsi.Raila Odinga ni mshindani anayestahili, namtakia kila la kheri kwa sababu kesho itakuwa wazi kuwa siku yake ya jua," Amesema Mudavadi.