Baba ya DJ Evolve akana madai kwamba alinunuliwa ili kutupilia kesi dhidi ya Babu Owino

Muhtasari

• Bw. Orinda alipuuzilia mbali madai kwamba alinunuliwa ili familia yake ikubali kuondolea mbunge huyo wa Embakasi Mashariki mashtaka.

•Bw Orinda alisema hawangenufaika kwa chochote iwapo Babu Owino angefungwa gerezani na mwanawe  aangamie kutokana na madhara ya risasi aliyompiga.

Baba ya DJ Evolve John Orinda katika studio za Radio Jambo
Baba ya DJ Evolve John Orinda katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Baba wa mcheza santuri Felix Orinda almaarufu kama DJ Evolve, John Orinda amejitokeza kuzungumzia hatua ya mwanawe kuondoa kesi ya jaribio la mauaji dhidi ya Babu Owino.

Akiwa kwenye mahojiano na Standard, Bw. Orinda alipuuzilia mbali madai kwamba alinunuliwa ili familia yake ikubali kuondolea mbunge huyo wa Embakasi Mashariki mashtaka.

Orinda alisema amepatia afya ya mwanawe kipaumbele  huku akieleza walifanya maamuzi ya kutafuta suluhu nje ya mahakama ili kuangazia kumhudumia mwanawe baada ya mkewe kuaga dunia.

"“Nasikia baadhi ya watu wakidai kwamba nilibadilisha kesi ya mwanangu na pesa. Kwani wananichukulia vipi? Kama mtu asiye na huruma na ambaye angeuza hali ya afya ya mwanawe?" Bw Orinda alisema.

Bw Orinda aliendelea kusema hawangenufaika kwa chochote iwapo Babu Owino angefungwa gerezani na mwanawe  aangamie kutokana na madhara ya risasi aliyompiga.

"Watu wana haki ya kutoa maoni yao. Kwangu mimi, afya ya mwanangu inapiku masuala mengine yote. Najua kuna watu ambao wangetamani kumuona Babu Owino gerezani. Lakini, tungefaidika nini?" Alihoji Bw Orinda.

Siku ya Jumanne mahakama ilikubali wasilisho la DJ Elvolve la kumuondolea mbunge Babu Owino mashtaka ya jaribio la mauaji yaliyokuwa yanamkabili mahakamani.

DJ Evolve alikubali kuondoa mashtaka dhidi ya mbunge huyo wa muhula wa kwanza kufuatia suluhisho la nje ya mahakama.

Hata hivyo, Babu atashtakiwa katika shtaka la pili la kujiendesha kwa fujo huku akiwa amebeba bunduki.

Katika juhudi za kutafuta suluhu nje ya mahakama, Babu alijitolea kumnunulia DJ Evolve nyumba pamoja na ahadi zingine kochokocho.