Watu wawili wafariki katika visa vya moto Nairobi

Muhtasari

•Mmoja alifariki katika kisa cha moto kilichotokea eneo la Riruta huku mwingine akiangamia katika kisa kilichoripotiwa katika eneo la Juakali.

•Wahasiriwa ambao nyumba zao ziliteketea waliomba malazi katika makanisa ya mitaani huku wakiomba usaidizi wa kujenga makazi mapya.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Watu wawili waliangamia katika visa viwili tofauti vya moto vilivyotokea jijini Nairobi wikendi ambayo imetamatika.

Mmoja alifariki katika kisa cha moto kilichotokea eneo la Riruta huku mwingine akiangamia katika kisa kilichoripotiwa katika eneo la Juakali.

Polisi wamesema takriban nyumba hamsini ziliharibiwa katika mikasa hiyo ya moto na kuacha makumi ya watu bila makao.

Watu kumi walijeruhiwa katika matukio hayo ya usiku wa Jumapili.

Uchunguzi wa kubaini chanzo cha mioto ile unaendelea huku mili ya waliofariki ikihifadhiwa katika mochari tofauti Nairobi.

Walioshuhudia walisema miili ya wawili ambao waliangamia ilipatikana baada ya mioto kuzimwa.

Wahasiriwa ambao nyumba zao ziliteketea waliomba malazi katika makanisa ya mitaani huku wakiomba usaidizi wa kujenga makazi mapya.

Walisema walipoteza mali yao kwa moto.

Watu watano walijeruhiwa walipokuwa wanakimbia kuokoa mali yao.

Bosi wa polisi jijini Nairobi James Mugera amesema polisi wanachunguza kubaini chanzo cha mioto hiyo.

Alisema mara nyingi shughuli ya kudhibiti visa kama vile hutatizwa na hali mbaya ya barabara katika maeneo hayo.

Alisema kwamba takriban visa viwili vya moto huripotiwa kila siku jijini Nairobi.