Sitajiuzulu ili kuwania kiti cha kisiasa- Waziri Kagwe aapa

Muhtasari

•Kagwe alisema kuwa amekuwa akiwazia suala la kuwania kiti cha kisiasa ila akaamua kutochukua hatua hiyo.

•Kagwe alisema hana tatizo lolote na mawaziri wengine pamoja na watumishi wa umma wanaojiuzulu ili kuwania viti vya kisiasa.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe
Image: Mercy Mumo

Huku mawaziri na wafanyikazi wengi wa serikaliwanaolenga kuwania viti vya kisiasa wakiendelea kujiuzulu ili kuangazia kampeni, waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kwamba hataondoka serikalini.

Tume ya uchaguzi nchini, IEBC ilitangaza Februari 9 kama siku ya mwisho kwa watumishi wote wa umma wanatazamia kuwania viti vya kisiasa kujiuzulu.

Siku ya Jumanne waziri Kagwe alisema kuwa amekuwa akiwazia suala la kuwania kiti cha kisiasa ila akaamua kutochukua hatua hiyo.

"Hapana, sitajiuzulu. Nimefikiria jambo hilo sana" Kagwe alisema.

Kagwe alisema itakuwa vibaya kwake kuacha Wakenya katika wakati huu mgumu wa janga la Covid-19 ambapo anahudumu kama waziri wa Afya.

"Niliitwa kwa serikali hii zaidi ya miaka miwili iliyopita na Rais Uhuru Kenyatta kuhudumu katika wadhifa huu mahususi. Nilikuwepo wakati Covid-19 ilipotukumba na bado nipo," Kagwe alisema.

"Bado tunapambana na janga hili, na sidhani kama itakuwa sawa kwa upande wangu kuachana na kaziwakati huu muhimu kwenda kugombea nafasi ya kuchaguliwa."

Kagwe aliahidi kusalia serikalini licha ya mawaziri wengine kujiuzulu.

"Mradi ni furaha ya Rais nitumikie katika wadhifa huu, sijisikii kujiuzulu na kufanya kitu kingine chochote. Kama ninaweza kusalia nyuma na kuokoa maisha ya Wakenya wengine watano, utakuwa uamuzi uliofikiriwa vyema,” alisema.

Kagwe alisema hana tatizo lolote na mawaziri wengine pamoja na watumishi wa umma wanaojiuzulu ili kuwania viti vya kisiasa.

"Ni haki ya kila Kenya kwenda na kushiriki katika mchakato wa uchaguzi na kuwania kiti chochote," alisema.