Uhuru Kenyatta amemwidhinisha rasmi Raila Odinga kuwania urais

Muhtasari
  • Alisema kuwa kiongozi wa ODM anaelewa nchi inakoelekea, na kwa hivyo atakuwa na amani kumkabidhi vazi la uongozi
Rais Uhuru Kenyatta
Image: Andrew Kasuku

Rais Uhuru Kenyatta amemwidhinisha rasmi kinara wa ODM Raila Odinga kuwania urais.

Akiwahutubia wajumbe wa eneo la Mlima Kenya, Uhuru alihimiza jamii yake kuunga mkono ombi la Raila akisema ana masilahi bora kwa nchi.

Rais akimrejelea Naibu Rais William Ruto alisema hatakuwa na shida kumuunga mkono siku zijazo iwapo atafanya mageuzi.

"Ninawaomba muunge mkono Raila Odinga kwani ana nia njema kwa Nchi. "Kijana wangu atakapofanya mageuzi", tutamzingatia," Uhuru alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Uhuru kuiambia jamii yake hadharani kwamba kiongozi huyo wa ODM ndiye mrithi wake anayependelea.

Rais amekuwa akidokeza kumuunga mkono kiongozi huyo wa ODM bila kutaja moja kwa moja.

Katika mkutano wa Sagana III, Uhuru alikuwa na ujasiri kwa kusema kwamba Raila ndiye aliyefaa zaidi sio tu kwa eneo la Mlima Kenya bali Kenya kwa ukubwa.

Rais alisema amezidisha uchumi wa nchi tangu alipochukua hatamu kutoka kwa Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Alisema kuwa kiongozi wa ODM anaelewa nchi inakoelekea, na kwa hivyo atakuwa na amani kumkabidhi vazi la uongozi.

"Kibaki aliacha uchumi wa maana wa Sh5 trilioni, leo mtu ambaye nitamkabidhi serikali...na ni mtu huyo (akimaanisha sauti za Baba) Ndiyo!

"Yule nitakayeshughulikia serikali, na mmemtaja, nitamwachia uchumi wa Sh13 trilioni," Uhuru alisema.