Viongozi wakuu ODM wamzindua Raila Odinga kugombea urais

Muhtasari

• Viongozi wakuu katika chama cha ODM wamemteua Raila Odinga kama  mgombeaji wa kipekee katika uchaguzi wa Agosti tisa.

• Naibu mwenyekiti wa ODM, Wycliffe Oparanya na gavana wa Mombasa Ali Hassa Joho wote walifutilia mbali azma zao za kuwania urais na badala yake kumuunga mkono Raila Odinga.

Enos Teche
Enos Teche
Image: KWA HISANI

Viongozi wakuu katika chama cha ODM wamemteua Raila Odinga kama  mgombeaji wa kipekee katika uchaguzi wa Agosti tisa.

Uamuzi huo uliafikiwa na wakuu hao wa chama siku ya Ijumaa huku uamuzi huo ukitarajiwa kusisitizwa Jumamosi katika mkutano wa jumla wa wajumbe wa chama cha ODM, utakaofanyika katika ukumbi wa Kasarani.

Naibu mwenyekiti wa ODM, Wycliffe Oparanya na gavana wa Mombasa Ali Hassa Joho wote walifutilia mbali azma zao za kuwania urais na badala yake kumuunga mkono Raila Odinga.

Hassan Joho kwa upande wake alikiri kwamba huu ni wakati wa Odinga kuingia ikulu.

“Nilitaka kuwa rais na tayari nilikuwa nimewasilisha ombi langu kwa chama. Hata hivyo, baada ya kuangalia na kudadisi hali halisi, leo ninajiondoa rasmi katika kinyangányiro hicho,” Oparanya alisema.

Ikumbukwe kuwa chama cha ODM tayari kilikuwa kimetangaza kwamba kitashirikiana na Muungano wa Azimio tunapoelekea katika uchaguzi mkuu.

Kwa hali hiyo, sasa Raila Odinga atawania kiti cha urais kupitia tikiti ya Azimio, hii ikiwa ni baada ya uamuzi uliofanywa na viongozi wakuu katika chama cha ODM siku ya Ijumaa katika ukumbi wa BOMAS.

Ifahamike kwamba vyama vya Jubilee na ODM ndio waasisi wakuu wa muungano wa Azimio.

Mbunge wa Suna mashariki, Junet Mohammed alisema kwamba muungano huwa utazinduliwa rasmi katika wiki mbili zijazo.