Mwendesha bodaboda atiwa mbaroni kwa kupiga polisi ngumi kichwani, Nairobi

Muhtasari

•Mshukiwa alishambulia afisa ambaye alikuwa anashughulikia ajali iliyotokea Alhamisi jioni ambayo ilihusisha pikipiki yake na gari ndogo. 

•Wahudumu wengine wa bodaboda waliokuwa wamejumuika pale wanaonekana wakimzuia mshukiwa kuendelea kumshambulia afisa huyo huku wakionya dhidi ya kuwachafulia jina.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi jijini Nairobi wanamzuilia mwendesha bodaboda mmoja ambaye alimpiga afisa mwenzao ngumi ya kichwa katika barabara ya Bunyala.

Mshukiwa alishambulia afisa anayetambulishwa kama Mark Muriira ambaye alikuwa anashughulikia ajali iliyotokea Alhamisi jioni. Ajali hiyo ilihusisha pikipiki ya mshukiwa na gari ndogo.

Mshukiwa ambaye alionekana kuwa mlevi alikamatwa papo hapo katika eneo la tukio na kupelekwa kituoni.

Katika video ambayo imekuwa ikienezwa mitandaoni, mwendesha bodaboda huyo ambaye alikuwa amevalia jaketi nyekundu na suruali ya buluu anaonekana akimgonga ngumi afisa huyo.

"Hakuna kusameheana hapa," Mwendesha bodaboda huyo anasikika akisema kabla ya kumgonga polisi huyo kichwani hadi kofia yake kuanguka.

Punde baada ya hayo, wahudumu wengine wa bodaboda waliokuwa wamejumuika pale wanaonekana wakimzuia mshukiwa kuendelea kumshambulia afisa huyo huku wakionya dhidi ya kuwachafulia jina.

"Wacha kupiga askari wewe. Anatuharibia jina hapa!," Wanaboda hao wanasikika wakiambia mwenzao.

Polisi aliyeshambuliwa anaonekana akimfuata nyuma mshukiwa na kuomba usaidizi kwa maafisa wenzake.

"Huyu jamaa amegonga mtu na pikipiki alafu ananipiga," Afisa huyo anaambia wenzake kabla ya mshukiwa kuwekwa pingu.

Jamaa huyo anawezwa nguvu na kikundi cha maafisa kilichokuwa pale na kuangushwa chini. Baadae aliandamana na maafisa wale hadi kituoni alikozuiliwa.