MCK yadai uchunguzi ufanyike baada ya mwanahabari kuvamiwa

Omwoyo ametoa wito wa uchunguzi wa haraka na kwamba mamlaka inapaswa kuwaona washukiwa hao wakifikishwa mahakamani.

Muhtasari
  • MCK yadai uchunguzi ufanyike baada ya mwanahabari kuvamiwa
Mkurugenzi mkuu wa MCK, David Omwoyo
Image: MCK (Facebook)

Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) limetaka uchunguzi ufanyike mara moja kuhusu madai ya shambulio dhidi ya Ian Byron, mwanahabari anayefanya kazi na Nation Media Group.

Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK David Omwoyo kwenye taarifa Jumanne alibainisha kuwa mwanahabari huyo alishambuliwa na watu wasiojulikana Jumapili katika kituo cha biashara cha Kakrao, kaunti ya Migori.

Baraza hilo lilisema kuwa shambulio hilo linajiri siku chache baada ya Byron kuripoti dhuluma kufuatia hadithi aliyoangazia Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed na jambo hilo kumfanya mbunge huyo kukosa amani.

Omwoyo ametoa wito wa uchunguzi wa haraka na kwamba mamlaka inapaswa kuwaona washukiwa hao wakifikishwa mahakamani.

Bw. Omwonyo aliendelea kubainisha kuwa tume hiyo inakatisha tamaa kesi za kushambuliwa kwa wanahabari na kuwataka watendaji wote ambao wanaweza kuwa waathiriwa wa shambulio hilo kuripoti zaidi suala hilo.

Pia alitoa wito kwa pande zote ambazo zinaweza kuathiriwa na kazi ya wanahabari kuripoti suala hilo kwa Tume ya Malalamiko ya Vyombo vya Habari.

"Baraza limebainisha kwa wasiwasi kuongezeka kwa visa vya mashambulizi yanayolenga wanahabari na mashirika ya habari kutoka kwa wanasiasa katika siku za hivi karibuni...Baraza limetoa wito kwa tasnia ya habari kuhakikisha mshikamano na usaidizi kwa wenzao walio katika dhiki,” aliandika Omwonyo.