IEBC yamtangaza Ruto rasmi kwenye gazeti la serikali

IEBC pia imemtangaza Rigathi Gachagua kuwa Naibu Rais mteule

Muhtasari

•IEBC imechapisha rasmi jina la William Ruto kwenye gazeti la serikali kama Rais mteule wa Jamhuri ya Kenya.

•Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati pia alichapisha jina la Rigathi Gachagua kuwa Naibu Rais mteule.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ampa rais mteule William Ruto cheti chake katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ampa rais mteule William Ruto cheti chake katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Image: ANDREW KASUKU

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imechapisha rasmi jina la William Ruto kwenye gazeti la serikali kama Rais mteule wa Jamhuri ya Kenya.

Katika notisi ya Agosti 16, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati pia alichapisha jina la Rigathi Gachagua kuwa Naibu Rais mteule.

Haya yanajiri kupitia matukio ya Jumatatu, ambapo Ruto alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkali wa Agosti 9, mwaka huu.

Ruto alipata kura 7,176,141, dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura 6,942,930 ambayo ni asilimia 48.85 ya kura.

Ruto alipata zaidi ya asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 39, na kupita idadi ya chini ya kaunti 24 zinazohitajika na Katiba. Raila alipata asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 34.

Haya yanajiri huku makamishna wanne wa IEBC wakipinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Wanne hao wakiongozwa na kamishna Juliana Cherera walisema hawawezi kumiliki matokeo kwa sababu ya hali ya kutoeleweka ambayo imekuwa ikishughulikiwa.

"Tumeufanya uchaguzi mkuu wa 2022 kwa ufanisi zaidi, tumehakikisha changamoto zote kudhibitiwa... Tumehakikisha kuwa kuboresha na tunasema ukweli kama makamishna tumekamilisha. kazi nzuri.

"Lakini baadhi ya mambo yanatakiwa kufanywa wazi kwani unaona sisi tuko hapa na sio Bomas ambapo matokeo yanaenda kutangazwa kwa sababu ya hali ya kutoeleweka ya jinsi awamu ilivyoshughulikiwa," Cherera alisema.

"Kwa hivyo hatuwezi kuchukua umiliki wa matokeo haya ambayo yanaenda kutangazwa," alitangaza.

Mwenyekiti wa IEBC alikuwa ameandamana na wenzake watatu Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang'aya.