Raila kuhutubia taifa leo Jumanne saa nane alasiri baada ya kupoteza uchaguzi

Raila ambaye aliwania kwa mara ya tano aliibuka wa pili katika kinyang'anyiro cha mwaka huu, nyuma ya Ruto wa UDA.

Muhtasari

•Dennis Onsarigo alisema waziri huyo mkuu wa zamani atatoa hotuba yake mwendo wa saa nane.

•Raila ambaye aliwania kwa mara ya tano aliibuka wa pili katika kinyang'anyiro cha mwaka huu, nyuma ya Ruto wa UDA.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: HISANI

Mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Odinga atalihutubia taifa leo (Jumanne) alasiri katika kituo cha habari cha Azimio kilichopo KICC.

Kupitia barua ya mwaliko kwa vyombo vya habari, Katibu wa habari wa sekretarieti ya urais ya Raila, Dennis Onsarigo alisema waziri huyo mkuu wa zamani atatoa hotuba yake mwendo wa saa nane.

"Hotuba ya Kiongozi wa Muungano wa Azimio La Umoja Rt Raila Odinga kwa Taifa. Muda: 2PM Mahali: KICC, Azimio Media Center. Tafadhali toa huduma za habari," Barua hiyo ilisoma.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa waziri mkuu huyo wa zamani kuonekana hadharani tangu tume ya IEBC kutangaza matokeo ya urais ambapo alipoteza.

Jumatatu jioni mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza mgombea wa UDA William Ruto kuwa rais mteule kufuatia uchaguzi wa Agosti 9.

Kulingana na IEBC, Ruto alitwaa ushindi baada ya kuzoa kura 7,176,141  (50.49%) huku Raila ikiibuka wa pili kwa kura 6,942,930 (48.85%).

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, DP Ruto alidai kuwa aliwasiliana na mshindani huyo wake kabla ya matangazo ya matokeo.

Rais mteule alifichua kuwa mazungumzo yake na Raila Jumatatu asubuhi kwa njia ya simu  yalihusu jinsi ya kuelekeza nchi ambapo walikubaliana kudumisha amani licha ya matokeo.

"Kama Mwanademokrasia, labda nifichue kwamba asubuhi ya leo, nilimpigia simu mshindani wangu mheshimiwa Raila Odinga na nikafanya mazungumzo naye," alisema.

"Tulikubaliana kwamba kwa vyovyote vile matokeo ya uchaguzi huu, tunapaswa kufanya mazungumzo."

DP alifichua hayo katika mahojiano na vyombo vya habari Jumatatu jioni, saa moja baada ya kutangazwa kuwa Rais Mteule.