Raila amsuta Ruto kuwawinda wabunge wa Azimio

Mutua alisema mbinu hiyo inalenga kuirejesha nchi katika enzi ya KANU ambapo uhuru wa bunge hilo ulipuuzwa.

Muhtasari

• Makau Mutua alimshutumu kiongozi huyo wa UDA kwa 'kuwanunua' wabunge wake ili kuibua hisia zisizo na maana kwamba ana mamlaka zaidi.

•Mutua alisema hakuna aliyeondoka, licha ya habari kwamba wanachama na chama wamegura timu ya Raila Odinga.

Makau Mutua, kinara wa ODM Raila Odinga, Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, na Mgombea mwenza wa Raila Martha Karua.
Makau Mutua, kinara wa ODM Raila Odinga, Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, na Mgombea mwenza wa Raila Martha Karua.
Image: FACEBOOK// MAKAU MUTUA

Sekretarieti ya urais ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya imemsuta Rais mteule William Ruto kwa 'kuwawinda' wabunge wake.

Katika taarifa yake Ijumaa, msemaji wa sekretarieti Makau Mutua alimshutumu kiongozi huyo wa UDA kwa 'kuwanunua' wabunge wake ili kuibua hisia zisizo na maana kwamba ana mamlaka zaidi.

"Tumeshtushwa kwamba Naibu Rais William Ruto, ambaye ana ndoto za kuongoza Kenya, tayari anajihusisha na vitendo vya kutokujali na kupuuza utawala wa sheria," msemaji wa Azimio Makau Mutua alisema katika taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa mbinu hiyo inalenga kuirejesha nchi katika enzi ya KANU ambapo uhuru wa bunge hilo ulipuuzwa.

"Anapaswa kujua demokrasia inahitaji wingi wa watu wengi ambapo vyama tofauti vya siasa vinashindana katika masuala. Majaribio ya kula Azimio kwa kufisidi wanachama wake hayatafanikiwa," alisema, akibainisha kuwa Hati ya Makubaliano ya Azimio inawafunga wanachama wote kwenye Muungano.

"Kuna miongozo iliyo wazi. Ruto anapaswa kujua kuwa ni kinyume cha sheria kwake, au kwa wengine, kuwashawishi wanachama kuondoka Azimio."

Mutua alisema hakuna aliyeondoka, licha ya habari kwamba wanachama na chama wamegura timu ya Raila Odinga.

"Hakuna mwanachama wa Azimio ambaye ameomba kisheria mchakato wa kujiondoa katika umoja huo. Wanachama wote waliotia saini kama wanachama wa awali bado ni wanachama wenye hadhi nzuri. Kwa hiyo, kasoro yoyote inayodaiwa kuwa ni batili kisheria."

Mutua alizidi kumsuta Ruto akisema tayari anapuuza utawala wa sheria licha ya kuahidi kuufuata.

Alidokeza kuwa demokrasia ambayo Kenya inafurahia inaamuru vyama vyote vya kisiasa kushindana katika masuala mbalimbali.

Wakili huyo alimtaka Ruto akome kujihusisha na kile alichokitaja "utamaduni wa ufisadi wa kisiasa".

Aidha alionyesha imani kuwa uamuzi wa mahakama utaupendelea Muungano huo.

"Mahakama itakuwa mwamuzi wa mwisho wa nani alishinda uchaguzi huu, na tuna imani kwamba tulishinda."

"Kwa nini Ruto ameingiwa na woga na kuendekeza mienendo haramu na ya ufisadi katika ukiukaji wa sheria? Inaweza kuwa tu kwa sababu amehisi kushindwa".

Mutua aliwataka viongozi wote wa Azimio na Independent waliochaguliwa kuepuka kuhama.

"Tunawaomba wafuasi wetu na wale waliochaguliwa kwenye Azimio, au kama Wanaojitegemea, kusimama kidete kutetea demokrasia yetu."

(Utafsiri: Samuel Maina)