Chebukati kuongoza makamishna kutoa heshima za mwisho kwa msimamizi wa uchaguzi aliyeuawa

Marehemu Daniel Musyoka atazikwa katika kijiji cha Muuani, wadi ya Muthetheni, kaunti ndogo ya Mwala.

Muhtasari

•Inatarajiwa kuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi pia watahudhuria.

•Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11 saa nne kasorobo asubuhi na mwili wake ukapatikana siku nne baadaye huko Mariko, eneo la  Loitoktok, Kaunti ya Kajiado.

Daniel Musyoka
Daniel Musyoka
Image: MAKTABA

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Ijumaa ataongoza makamishna sita katika kutoa heshima zao za mwisho kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Embakasi Mashariki Daniel Musyoka.

Inatarajiwa kuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi pia watahudhuria.

Kulingana na IEBC, tume hiyo ikijumuisha wafanyikazi wake itakutana mwendo wa saa tatu asubuhi katika Mochari ya Montezuma huko Machakos kisha kuelekea Kijiji cha Muuani, wadi ya Muthetheni, kaunti ndogo ya Mwala kwa mazishi.

Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11 saa nne kasorobo asubuhi na mwili wake ukapatikana siku nne baadaye huko Mariko, eneo la  Loitoktok, Kaunti ya Kajiado.

Chebukati aliomba uchunguzi ufanyike haraka kuhusu mauaji na kufunguliwa mashtaka kwa waliohusika.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya Msimamizi wa Uchaguzi wa IEBC.