Makamishna wanne 'waasi' wa IEBC wapata pigo

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amepata ushindi katika raundi ya kwanza ya kesi ya urais.

Muhtasari

•Mrengo unaoongozwa na Juliana Cherera ulikuwa umemwasilisha mbele ya mahakama hiyo Wakili Paul Muite kama wakili wa IEBC.

Makamishna Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya.
Makamishna Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya.
Image: FREDRICK OMONDI

Mahakama ya Juu imetupilia mbali majibu yaliyowasilishwa kwa niaba ya shirika la uchaguzi na makamishna wanne wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera, na kutoa ushindi wa mapema kwa mwenyekiti Wafula Chebukati.

Akizungumza Jumanne wakati wa kikao cha pili cha malalamishi ya kesi ya uchaguzi wa urais ya 2022 katika Mahakama ya Milimani, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alisema mahakama imemuamuru Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai, ambaye anawakilisha kundi la Chebukati kuwa wakili anayewakilisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika suala hilo.

Mrengo unaoongozwa na Juliana Cherera ulikuwa umemwasilisha mbele ya mahakama hiyo Wakili Paul Muite kama wakili wa IEBC.

Lakini mwendo wa alasiri, mahakama iliwapatia pigo makamishna wanne -- Bi Cherera, Bi Irene Masit, Bw Justus Nyang'aya na Bw Francis Wanderi -- huku ikifafanua kuwa wako huru kuhifadhi huduma za Bw Muite na Issa Mansu kwa muda wa kesi hiyo.

Katika kikao cha asubuhi, mawakili wote wawili walikuwa wamesisitiza kuwa wanawakilisha IEBC katika ombi la kupinga uchaguzi wa urais lililowasilishwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

Mrengo unaoongozwa na Cherera ulikuwa umewasilisha jibu kwa niaba ya IEBC iliyotaka kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyomtangaza William Ruto kuwa Rais mteule.

Katika usomaji wa awali wa uamuzi wa mahakama, Jaji Mwilu alikuwa amewataka makamishna wanaogombana wa shirika la IEBC kutatua mizozo yao ya ndani nje ya mahakama. Bi Mwilu alikuwa amesema mahakama haitajiingiza katika suala la kuamua ni wakili gani atawakilisha IEBC.