Msichana wa kidato cha 3 ajitoa uhai baada ya kudaiwa kuiba Sh 2,500

Msichana huyo alishtumiwa kwa kuibaSh2,500 ambazo zilikuwa pesa za mfukoni za mwanafunzi mwenzake.

Muhtasari

•Mwili wa marehemu ulipatikana ukining'inia kutoka kwenye mbao ya choo katika shule moja eneo hilo.

•Uchunguzi wa tukio hilo pia umeanzishwa.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Msichana wa kidato cha tatu aliripotiwa kufariki kwa kujitoa uhai huko Matungulu, Kaunti ya Machakos mnamo Jumatano.

Naibu kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Matungulu Evans Mose alisema mwili wa marehemu ulipatikana ukining'inia kutoka mbao ya choo katika shule moja eneo hilo.

Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Tala mwendo wa saa tisa na dakika arubaini siku ya Jumatano.

Alisema msichana huyo alishtumiwa kwa kuibaSh2,500 ambazo zilikuwa pesa za mfukoni za mwanafunzi mwenzake.

"Alitajwa vkama mshukiwa na wenzake wengi wakati suala hilo lilipokuwa likichunguzwa," Mose alisema kwa simu siku ya Alhamisi.

"Marehemu alikiri kwamba aliiba pesa hizo na alikuwa amezihifadhi kwenye bweni."

Alisema mwanafunzi huyo aliambiwa na mwalimu atoe fedha alizozificha wakati wa mapumziko na kupatia uongozi wa shule.Ni wakati huo ambapo inasemekana marehemu alipanga njama ya kukatisha maisha yake.

"Msichana huyo alipewa funguo za bweni lakini alikosa kurejea. Hii ilimfanya naibu mkuu wa shule kwenda kumtafuta. Kwa bahati mbaya, walipata mwili wa msichana ukining'inia kutoka kwenye paa la choo ndani ya jengo la bweni," Mose alisema.

Polisi waliuhamisha mwili huo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kangundo level 4, ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Uchunguzi wa tukio hilo pia umeanzishwa.