Fuliza! Ada ya mikopo ya fuliza yapunguzwa kwa 50%

Hakuna ada itakayotozwa wateja wanaokopa chini ya Shilingi 1,000 kwa siku tatu za kwanza.

Muhtasari

• Hatua hii inatarajiwa kunufaisha angalau asilimia 80 ya wakopaji milioni 28 kwenye jukwaa ambalo lilizinduliwa na Safaricom na benki hizo mbili mwaka 2019.

Mashirika ya Safaricom, KCB na NCBA yamefutilia mbali ada za utunzi wa mfumo zilizokuwa zikitozwa wateja wa Fuliza wanaokopa chini ya Shilingi 1,000 kwa siku tatu za kwanza.

Hatua hii inatarajiwa kunufaisha angalau asilimia 80 ya wakopaji milioni 28 kwenye jukwaa ambalo lilizinduliwa na Safaricom na benki hizo mbili mwaka 2019.

Akizungumza wakati wa mkutano uliohudhuriwa na Rais William Ruto, Afisa mkuu mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa alitangaza kupunguzwa kwa ada za mkopo wa Fuliza kwa asilimia 50.

"Hii inatarajiwa kupunguza gharama za mikopo na ufikiaji kwa nusu kwa wateja wetu tunapotembea katika safari ya ujumuishaji wa kifedha," Ndegwa alisema.