Afisa wa polisi ajiua kwa kujipiga risasi, Gilgil

Konstebo John Wambua alipatikana akiwa amefariki baada ya kujipiga risasi kifuani

Muhtasari

• Chanzo cha cha afisa huyo kujitia kitanzi bado hakijabainika.

• Hakuna barua ya kujiua iliyopatikana ndani ya nyumba.

• Alikimbizwa katika hospitali ya Gilgil ambako ilitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Crime Scene
Image: HISANI

Polisi wanachunguza kisa ambapo afisa mmoja alijiua katika kambi ya Kitengo cha Kupambana na Wizi wa mifugo huko Eburu, Gilgil.

Konstebo John Wambua alipatikana akiwa amefariki baada ya kujipiga risasi kifuani siku ya Jumatano, Septemba 28 mwendo wa saa mbili usiku.

Polisi walisema Wambua alijifungia chumbani mwake na kujipiga risasi kifuani.

Chanzo cha cha afisa huyo kujitia kitanzi bado hakijabainika.

Wenzake walisikia mlio wa risasi kutoka kwa nyumba yake na walipokwenda kuangalia walimkuta akiwa amelala kwenye dimbwi la damu huku bunduki ikiwa kando ya mwili.

Walioshuhudia walisema maafisa walilazimika kuvunja mlango wa nyumba hiyo ili kuingia ndani kwani alikuwa amejifungia ndani.

Alikimbizwa katika hospitali ya Gilgil ambako ilitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Hakuna barua ya kujiua iliyopatikana ndani ya nyumba.

Hili ni tukio la hivi punde la afisa wa polisi kujiua.

Makumi ya maafisa wa polisi wamekufa kutokana na kujitoa uhai, hali ambayo inahusishwa na msongo wa mawazo kazini.