Gavana Wanga afichua kwa nini hakumpokea rais William Ruto huko Homa Bay

Wanga hakuungana na rais Ruto kuabudu katika kanisa la Homa Bay AIC.

Muhtasari

•Jumapili asubuhi rais aliungana na waumini wa kanisa la AIC Homa Bay kwa ibada kabla ya kuhutubia wakazi wa kaunti hiyo baadae.

•Gavana Gladys Wanga hakuwepo kumpokea rais katika kaunti yake kama ilivyo tamaduni ya magavana wengine.

katika kanisa la Homa Bay AIC mnamo Septemba 2, 2022.
Rais William Ruto pamoja na viongozi wa kidini katika kanisa la Homa Bay AIC mnamo Septemba 2, 2022.
Image: ROBERT OMOLLO

Leo hii, Jumapili ya Oktoba 2, 2022, rais William Ruto yuko katika kaunti ya Homa Bay.

 Hii ni ziara ya kwanza ya Ruto katika eneo la Nyanza  baada ya kuapishwa kuwa rais wa tano wa Kenya.

Jumapili asubuhi rais aliungana na waumini wa kanisa la AIC Homa Bay kwa ibada kabla ya kuhutubia wakazi wa kaunti hiyo baadae.

Hata hivyo gavana Gladys Wanga hakuwepo kumpokea rais katika kaunti yake kama ilivyo tamaduni ya magavana wengine.

Katika taarifa aliyotoa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, gavana Wanga ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama pinzani cha ODM kuwa kwa sasa yupo kwenye ziara ya kikazi nje ya kaunti ya Homa Bay.

Gavana huyo hata hivyo alisema kuwa rais yuko karibu sana katika kaunti yake na kumtaka ajihisi nyumbani.

"Rais Dkt William Ruto leo tarehe 2 Oktoba 2022 ameratibiwa kuzuru Mji wa Homa Bay kuabudu nasi katika Kanisa la AIC. Ningependa kumkaribisha Rais kwa niaba ya watu wa Homa Bay na kumuomba ajisikie yuko nyumbani. Hata hivyo niko nje ya kaunti kwa kazi rasmi na kwa hivyo sitaweza kujiunga na rais kwa ibada ya kanisa na nimewasiliana naye kuhusu hilo," alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Gavana huyo wa muhula wa kwanza alidokeza kuwa yupo katika kaunti ya Mombasa.

Alibainisha kuwa wakazi wa Homa Bay wako tayari kumpa rais mapokezi mazuri.

"Watu wa Homa Bay wana utamaduni wa ukarimu mkubwa na watampokea Rais kwa furaha anapotutembelea kusali nasi. Karibu sana," alisema.

Ziara ya rais katika kaunti ya Homa Bay inajiri wiki chache tu baada ya naibu wake Rigathi Gachagua kuzuru kaunti jirani ya Kisumu.

Mnamo Septemba 23, DP Rigathi Gachagua alikuwa Kisumu kuongoza tamasha la tuzo za Kenya Music Festival na alipokewa na gavana Anyang' Nyong'o na waziri wa elimu George Magoha miongoni mwa viongozi wengine.

Katika uchaguzi wa Agosti 9, Ruto na Rigathi walipata kura finyu sana kutoka eneo la Nyanza  linaloaminika kuwa ngome la Raila Odinga.