Bilionea! Musalia Mudavadi afunguka kuhusu utajiri wake mkubwa

Waziri Mkuu Mteule huyo alifichua kuwa ana thamani ya Sh4 bilioni.

Muhtasari

•"Nikichukua uwekezaji wangu katika hisa katika baadhi ya makampuni na pia mali ninazomiliki nitataja thamani yangu kuwa takriban Sh4 bilioni," alisema.

•Naibu Waziri Mkuu huyo wa zamani ndiye wa kwanza kukabiliana na jopo la uhakiki.

Waziri Mkuu Mteule Musalia Mudavadi
Image: MAKTABA

Waziri Mkuu Mteule Musalia Mudavadi amefichua utajiri wake, huku akikabiliana na Kamati ya Uteuzi kwa ajili ya uhakiki.

Akizungumza huko bungeni siku ya Jumatatu , Mudavadi alifichua kuwa ana thamani ya Sh4 bilioni.

"Nikichukua uwekezaji wangu katika hisa katika baadhi ya makampuni na pia mali ninazomiliki nitataja thamani yangu kuwa takriban Sh4 bilioni," aliambia jopo la uhakiki.

Aliongeza kuwa mapato yake ya sasa na anayotarajia ni kutoka kwa mapato ya kukodisha, mgao wa hisa, riba na mapato mengine yaliyotokana na shamba.

Naibu Waziri Mkuu huyo wa zamani ndiye wa kwanza kukabiliana na jopo la uhakiki.

 Wateule wengine wanaokadiriwa kuchunguzwa Jumatatu ni pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye ndiye mteule wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Aden Duale (Ulinzi), Alfred Mutua (Masuala ya Kigeni na Diaspora) na Alice Wahome (Maji, Usafi na Unyunyizaji maji).

 Chini ya Agizo la Utendaji Na.1 la 2022, Rais William Ruto alibainisha kwa uwazi majukumu ya mwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na kushughulikia Kitengo cha Uwasilishaji Serikalini.

Zaidi ya kumsaidia Rais na Naibu Rais katika uratibu na usimamizi wa Wizara na Idara za Serikali, majukumu muhimu ya Waziri Mkuu  ni pamoja na; Kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Utawala wa Kitaifa katika kusimamia utekelezaji wa sera, programu na miradi ya Serikali ya Kitaifa pamoja na usimamizi na uratibu wa ajenda za sheria za Serikali ya Kitaifa katika wizara na idara zote za serikali kwa ajili ya kupitishwa kwa viongozi wa muungano Bungeni.

 Mudavadi pia atapewa jukumu la kuongoza Kamati za Makatibu Wakuu na kusimamia ufuatiliaji wa kitaalamu na tathmini ya sera, programu na miradi ya Serikali.

Nafasi ya mwisho ya Mudavadi katika serikali ilikuwa ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Serikali ya Mitaa kati ya 2008 hadi 2013 katika Serikali ya Muungano Mkuu wakati wa uongozi wa marehemu Mwai Kibaki.