Sakaja:Sitafunga makanisa yenye kelele

Siku ya Jumapili, kasisi wa Kikatoliki alimwomba Sakaja kufikiria kufunga makanisa yenye kelele

Muhtasari
  • Badala yake, alisema, kaunti itafanya mazungumzo nao kuhusu kuzingatia sheria na kanuni, ili waendelee kueneza injili
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Image: Facebook

Gavana wa Kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amesema hatafunga makanisa yenye kelele katika maeneo ya makazi ya jiji.

Badala yake, alisema, kaunti itafanya mazungumzo nao kuhusu kuzingatia sheria na kanuni, ili waendelee kueneza injili.

Akizungumza siku ya Alhamisi wakati wa uzinduzi wa Kituo cha mabasi cha Green Park, Sakaja alidokeza kuwa hatarejelea uamuzi wake kuhusu baa na mikahawa.

"Sitarudi nyuma juu ya kufutwa kwa baa na mikahawa kutoka kwa makazi. Tumefunga sura hiyo. Tuendelee. Wanaosema watu watapoteza kazi wanatafuta huruma. Ni jambo sahihi kufanya ingawa halipendezi," alisema.

Siku ya Jumapili, kasisi wa Kikatoliki alimwomba Sakaja kufikiria kufunga makanisa yenye kelele, akisema makanisa mengine yana sauti zaidi kuliko vilabu.

"Nchi yetu ina kelele sana...leo makanisa yana kelele kuliko baa, huo ndio ukweli. Makanisa yetu yana kelele zaidi ya kunywa pombe. Hiyo inakuambia tuna shida," alisema.