Dereva wa Safari Rally Asad Khan kuzikwa leo Jumatatu

Familia ya Asad ilitangaza kifo chake siku ya Jumapili jioni.

Muhtasari

•Kwa mujibu wa mpango wa mazishi, mazishi ya marehemu Asad yatafanyika katika Msikiti wa Parklands ulioko 3rd Parklands.

•Marehemu alikuwa amelazwa hospitalini kwa takriban wiki moja na familia ilikuwa imetoa ombi la damu.

Marehemu Asad Khan
Image: HISANI

Dereva mkongwe wa Safari Rally wa Kenya, marehemu Asad Khan atazikwa leo (Disemba 19) jioni katika makaburi ya Waislamu ya Kariokor.

Kwa mujibu wa mpango wa mazishi, mazishi ya marehemu Asad yatafanyika katika Msikiti wa Parklands ulioko 3rd Parklands kabla ya swala ya Asr ambayo itafanyika saa kumi jioni. Jumatatu. Baada ya maombi hayo, mwili wa marehemu utasafirishwa hadhi kwenye makaburi ya Kariokor ambako utazikwa.

Familia ya Asad ilitangaza kifo chake siku ya Jumapili jioni.

Kakake Khan, Adil alithibitisha kifo chake na kusema kuwa alifariki katika Hospitali ya Avenue, ambako alikuwa akipokea matibabu.

Asad alikuwa akipigania maisha yake katika kitengo cha wagonjwa wanaohitaji utegemezi wa hali ya juu cha hospitali hiyo kufuatia madai ya mzozo wa nyumbani na mpenzi wake Maxine Wahome ambao ulipelekea kukamatwa kwake.

Khan alikuwa amelazwa huko baada ya kupoteza damu nyingi kufuatia majeraha aliyoyapata katika nyumba yake ya Kileleshwa wakati wa mzozo huo. Mpenzi wa marehemu, Maxine pia ni dereva wa mbio za magari.

Adil alisema kaka yake alipoteza damu nyingi baada ya shambulio hilo la kinyama lililotokea Jumanne iliyopita mwendo wa asubuhi.

Marehemu alikuwa amelazwa hospitalini kwa takriban wiki moja na familia ilikuwa imetoa ombi la damu.

Kulingana na Adil, kaka yake alijeruhiwa na Maxine baada ya kudaiwa kurudi nyumbani akiwa amelewa kutoka kwenye karamu aliyokuwa amehudhuria.