Mama wa mshukiwa wa kumng'oa macho mtoto wa miaka 3 akamatwa Nairobi

Polisi walisema Pacifica Nyakerario alikamatwa katika eneo la Kasarani, Nairobi.

Muhtasari

•Polisi walimtafuta hadi kwenye nyumba ambayo amekuwa tangu siku mtoto Junior Sagini alipong'olewa macho.

•Alex Maina Ochogo alifikishwa mahakamani kuhusu kesi hiyo siku ya Jumatatu.

Pacifica, mama wa mshukiwa aliyeshtakiwa kwa kumng'oa macho mtoto, akisindikizwa kortini Kisii mnamo Desemba 20.
Pacifica, mama wa mshukiwa aliyeshtakiwa kwa kumng'oa macho mtoto, akisindikizwa kortini Kisii mnamo Desemba 20.
Image: THE STAR

Mshukiwa mwingine wa kumng'oa macho mvulana wa miaka mitatu katika kaunti ya Kisii alikamatwa Jumatatu usiku jijini Nairobi.

Polisi walisema Pacifica Nyakerario alikamatwa katika eneo la Kasarani, Nairobi.

Polisi walimtafuta hadi kwenye nyumba ambayo amekuwa tangu siku mtoto Junior Sagini alipong'olewa macho.

Haya yanajiri saa chache baada ya mwanawe Pacifica, Alex Maina Ochogo kufikishwa mahakamani kuhusu kesi hiyo.

Jumatatu usiku alihamishiwa Kisii ambapo uchunguzi unaendelea.

Pacifica aliwasilishwa katika mahakama ya Kisii Jumanne, Desemba 20 ambapo polisi walitaka azuiliwe ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi.

Ochogo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Christine Ogweno kwa kumng'oa macho mtoto wa miaka mitatu katika kijiji cha Ikuruma, kaunti ndogo ya Marani, Kaunti ya Kisii.

Kiongozi wa mashtaka Hilary Kaino alitoa ombi hilo tofauti la kuzuiliwa kwa mshukiwa kwa siku tano ili kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi na pia kuwakamata washukiwa zaidi akiwemo mamake Ochogo.

Kaino aliambia mahakama kuwa Ochogo alionekana akimsindikiza mama yake hadi kituo cha basi, ambaye kisha alikimbilia Nairobi siku ambayo Sagini alipatikana kwenye shamba la mahindi.

Polisi wanachunguza kesi ya jaribio la mauaji.

Ogweno aliamua kwamba mshukiwa atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Rioma kwa siku tano huku polisi wakikamilisha uchunguzi.

"Mshukiwa atafikishwa katika mahakama hiyo Desemba 23 ili kujua hatima yake huku mahakama ikitoa maelekezo," alisema Hakimu.