KCPE 2022: Watahiniwa wote watajiunga na shule ya Upili- Waziri Machogu

Machogu alisema serikali itaweka watahiniwa wote katika shule ya upili.

Muhtasari

• Machogu aliwatahadharisha wazazi kutowaweka watoto wao nyumbani wakati wa kujiunga na kidato cha kwanza.

•Machogu alisema watahiniwa 252 walinaswa wakijihusisha na udanganyifu katika vituo mbalimbali kote nchini.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE katika afisi za KNEC kando ya Barabara ya Dennis Pritt Kilimani, Nairobi mnamo Desemba 21, 2022.
Waziri wa elimu Ezekiel Machogu wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE katika afisi za KNEC kando ya Barabara ya Dennis Pritt Kilimani, Nairobi mnamo Desemba 21, 2022.
Image: ANDREW KASUKU

Watahiniwa wote wa KCPE 2022 ambao wamepokea matokeo yao wataweza kujiunga na shule ya upili, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ameahidi.

Alizungumza  siku ya Jumatano katika Mtihani House jijini Nairobi wakati wa matangazo ya matokeo ya mtihani, Machogu aliwatahadharisha wazazi kutowaweka watoto wao nyumbani wakati wa kujiunga na kidato cha kwanza.

"Watahiniwa wote ambao matokeo yao ninayotoa leo watakubaliwa katika kidato cha kwanza chini ya sera ya mpito wa asilimia 100," alisema.

Machogu alisema serikali itaweka watahiniwa wote katika shule ya upili.

Waziri huyo pia alibainisha kuwa watahiniwa waliohusika katika visa vya udanganyifu katika mitihani watapokea matokeo yao.

Kulingana na Machogu, hii itakuwa katika jitihada za kufikia mpito kamili wa kutoka shule ya msingi hadi shule ya upili.

“Watahiniwa watapata matokeo yao na watajiunga na shule ya upili. Hii ni katika ari ya mpito wa asilimia 100,” alisema.

Machogu alisema watahiniwa 252 walinaswa wakijihusisha na udanganyifu katika vituo mbalimbali kote nchini.

Aliongeza kuwa watahiniwa hao hawakupewa alama zozote katika mitihani ambayo walidanganya. 

“Kwa ujumla kulikuwa na watahiniwa 252 katika vituo tisa vya mitihani waliobainika kujihusisha na makosa. Watahiniwa hawa wamepata sifuri katika masomo ambapo walijihusisha na makosa. Hata hivyo, alama za jumla za wanafunzi walioathirika zitawekwa baada ya kuondolewa kwa alama za somo lililoathiriwa.”

Takriban watahiniwa 1,244,188 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambao ulifanyika Novemba 28 hadi 30.

Wanafunzi 9443 walifanikiwa kupata alama 400 kuenda juu. Watahiniwa wengine 307, 756 walipata kati ya alama 300 na 399.

Watahiniwa 619 593 walipata alama kati ya 200 na 299 huku 296,336 wakipata alama kati ya  100 na 199. Wanafunzi 724 walipata alama 99 kuenda chini.