Rafikiye Chiloba akamatwa kama mshukiwa mkuu katika mauaji ya mwanaharakati huyo

Mshukiwa anahojiwa ili kutoa taarifa zaidi juu ya mauaji hayo.

Muhtasari
  • Alisema polisi walikuwa wakikusanya taarifa za kijasusi kuhusu suala hilo na marehemu alitambulika kama Edwin Kiptoo almaarufu Chiloba
  • Mshukiwa ametambuliwa kwa jina Jacktone Odhiambo ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa marehemu
Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi mjini Eldoret wamemkamata mshukiwa mkuu ambaye ni mpiga picha wa kujitegemea anayeishi Nairobi kuhusiana na mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Kiprotich kiptoo almaarufu Chiloba.

Mshukiwa ametambuliwa kwa jina Jacktone Odhiambo ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa marehemu.

Polisi sasa wanawasaka washukiwa wawili waliosaidia kuupakia mwili wa Chiloba kwenye sanduku la chuma kabla ya kutupwa eneo la Halingham karibu na Kipkaren.

Kimulwo alisema kuwa baada ya uchunguzi marehemu alionekana kunyongwa na kung'olewa jicho moja.

Mkuu wa DCI kaunti ya Uasin Gishu Peter Kimulwo alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana.

Kimulwo alieleza kuwa polisi walikuwa wamearifiwa na chifu kwamba sanduku la chuma lilidondoshwa kando ya barabara eneo la Kipkaren mnamo Januari 3 2023.

Wakaazi walipata maiti ya mtu mzima ikiwa imefungwa kwa vazi la mwanamke kwenye sanduku la chuma

Hakukuwa na hati za utambulisho kwenye mwili huo na ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha MTRH huku uchunguzi ukiendelea.

Alisema polisi walikuwa wakikusanya taarifa za kijasusi kuhusu suala hilo na marehemu alitambulika kama Edwin Kiptoo almaarufu Chiloba.

Aliishi eneo la Kimmu na polisi walifuata eneo fulani ambapo waliwahoji wapangaji ambao walithibitisha kuwa anaishi katika chumba nambari 11 karibu na Noble Bliss Plaza. Marehemu alikuwa akiishi na wengine wawili.

Kimulwo alisema usiku wa kuamkia mwaka mpya Chiloba na marafiki zake walikwenda kwenye klabu ya Tamasha na walirudi saa 3 asubuhi walipokuwa wakiishi.

Walipofika majirani walisikia zogo na vilio vilipungua.

Majirani hawakufuatilia na marehemu hakuonekana lakini majirani wa 3 waliona gari likiwa na watu wawili wakipakia boksi la chuma kwenye gari na kuondoka.

Majirani walisema pia walisikia harufu mbaya kutoka kwa nyumba hiyo.

"Tunashuku kelele zilizosikika hapo awali na majirani ni wakati ambapo marehemu aliuawa", Kimulwo alisema.

Alisema DCI ilikuwa ikifuatilia gari lililotumika kutupa mwili huo.

Mshukiwa anahojiwa ili kutoa taarifa zaidi juu ya mauaji hayo.

Inasemekana kuwa washukiwa waliokamatwa waliwaambia majirani kwamba panya alikufa ndani ya nyumba hiyo baada ya majirani kutaka kujua kwa nini kulikuwa na uvundo kutoka kwa nyumba hiyo.

Hapo awali familia ya mwanaharakati wa LQBTQ Aliyeuawa Edwin Chiloba ilikuwa imetambua mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret.

Dada yake Melvin Faith na jamaa wengine wako katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo uchunguzi wa maiti utafanywa.