"Tafadhali mtuombee!" Wazazi wa mwanamitindo aliyeuawa Edwin Chiloba hatimaye wavunja kimya

Wamemuomboleza na kuandika jumbe za kihisia kufuatia kifo chake.

Muhtasari

•"Mioyo yetu imevunjika usiku wa leo. Tutatoa maelezo zaidi wakati tunaweza kusema zaidi. Tafadhali mtuombee.” wanandoa hao walisema.

•Edwin alikuwa yatima kwani wazazi wake halisi waliaga dunia katika nyakati tofauti hapo awali.

Edwin Chiloba na wazazi wake, Peter na Donna Pfaltzgraff
Image: HISANI

Wazazi walezi na wa kiroho wa mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Chiloba, Peter na Donna Pfaltzgraff wamemuomboleza na kuandika jumbe za kihisia kufuatia kifo chake. 

"Edwin, tunakupenda," Peter alisema kwenye mtandao wa Facebook.

"Mioyo yetu imevunjika usiku wa leo. Tutatoa maelezo zaidi wakati tunaweza kusema zaidi. Tafadhali mtuombee.” wanandoa hao walisema.

Waliandika haya baada ya kupata taarifa kwamba alikuwa ameuawa kikatili mjini Eldoret. Nia ya mauaji ya mwanamitindo huyo bado haijajulikana.

Peter na mkewe ambao ni wazungu walikuwa na uhusiano wa karibu sana na Chiloba na walimtaja kuwa mtoto wao wa kiroho.

Wanandoa hao wazee kutoka Marekani na ambao huendesha Huduma ya Grace and Faith Family Ministry waliashiria kutokuamini kwao kwa yaliyotokea, wakiomba maombi katika kipindi hiki.

Wawili hao walisapoti upendo wa Edwin wa mitindo kwa kumnunulia vifaa vya kuanza kazi yake kama muunda mitindo mwaka wa 2021.

"Utukufu ni kwa Mungu, kwa wazazi wangu wapendwa, kupata wazazi kama nyinyi kwa upande wangu kunanifanya niwe hivi nilivyo leo. Asanteni sana kwa kunisapoti bila masharti. Asanteni kwa kunisaidia kuunda maisha yangu kwa wema na shauku. Bila nyinyi, Nisingekuwa kama nilivyo leo. Asanteni kwa kila jambo, asanteni kwa kuniombea kila wakati na kunijenga kwa neno la Mungu. Siku moja nitawafanya mjivunie," alisema kwenye chapisho la Januari 2021. 

Mwili wa Chiloba uligunduliwa kwenye sanduku la chuma katika barabara ya Kipenyo-Katinga, kaunti ya Uasin Gishu na waendesha bodaboda, ambao waliona gari lisilo na nambari ya usajili likitupa sanduku hilo kando ya barabara.

Mshukiwa mkuu alikamatwa Ijumaa kwa mauaji hayo.

Polisi wanawasaka washukiwa wengine wawili. Mshukiwa alifahamika kama mshirika wa marehemu na alikuwa amesafiri hadi Eldoret kuungana naye kwa sherehe za Mwaka Mpya.

Polisi wanashuku pesa au mapenzi yaliyoenda mrama kuwa nia ya mauaji hayo.

Edwin alikuwa yatima kwani wazazi wake halisi waliaga dunia katika nyakati tofauti hapo awali.