Washukiwa 3 zaidi wakamatwa kuhusiana na mauaji ya Edwin Chiloba

3 hao ni vijana, wawili kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.

Muhtasari

•Watatu hao walikamatwa kwa kusaidia kubeba kisanduku cha chuma ambacho kilitumika kutupa mwili wa Chiloba.

•Mshukiwa alisema alimuua Chiloba ili kulipiza kisasi kwa kumsaliti.

Jackton Odhiambo na Edwin Chiloba
Image: INSTAGRAM

Washukiwa wengine watatu walikamatwa siku ya Jumamosi katika uchunguzi wa mauaji ya kikatili ya mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Kiprotich Kiptoo almaarufu Chiloba.

Hii inafikisha idadi ya washukiwa walio chini ya ulinzi kuwa wanne, polisi walisema.

Watatu hao walikamatwa kwa kusaidia kubeba kisanduku cha chuma ambacho kilitumika kutupa mwili wa Chiloba.

Watatu hao ni vijana, wawili kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, polisi walisema.

Msemaji wa polisi Resla Onyango alisema maafisa wa upelelezi pia wamezuilia gari ambalo lilitumika kutupa mwili huo barabarani.

Aliongeza kuwa mzozo wa kimapenzi ni miongoni mwa nadharia wanazofuatilia kwa sasa.

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanamitindo Jackton Odhiambo, 24, alikiri kumuua mwanamitindo huyo kwa madai kuwa alimsaliti kimapenzi.

Polisi walifichua kwamba Jackton alitekeleza mauaji hayo kwa usaidizi wa marafiki zake wawili.

Mshukiwa alisema alimuua Chiloba ili kulipiza kisasi kwa kumsaliti.

Jackton ambaye alikuwa amekaa na marehemu kwa mwaka mmoja mjini Eldoret alikamatwa siku ya Ijumaa kama mshukiwa mkuu wa mauaji hayo. Wawili hao waliishi pamoja kama mume na mke.

Msimamizi wa nyumba ambayo Chiloba alikuwa amepanga, Alex Nyamweya alisema kuwa Jackton alimpigia simu akitumia simu ya Chiloba mnamo Januari 4, na kumwarifu kwamba alikuwa akihama nyumba waliyokuwa wakiishi.

Polisi walisema Jackton aliondoka kwenye nyumba hiyo mara moja.

Jackton ni mpiga picha wa kujitegemea anayeishi Nairobi na alikuwa amejiunga na marehemu kwa sherehe za Mwaka Mpya.

Polisi walifichua kuwa Jackton aliwaambia majirani waliokuwa na hamu ya kutaka kujua harufu mbaya kutoka kwa nyumba aliyokaa Chiloba na wengine wawili kwamba ni panya aliyekufa na alikuwa akijaribu kuiondoa.

"Aliwaambia majirani ni panya aliyekufa ambaye alikuwa akinuka walipotaka kujua nini kilikuwa kinanuka kutoka kwa nyumba waliyokuwa wakiishi," mkuu wa DCI kaunti ya Uasin Gishu Peter Kimulwo alisema.

Mwili huo ulitupwa eneo la Halingham karibu na Kipkaren.

Majirani walikuwa wamemwona Jackton akiwa na sanduku la chuma siku moja mapema. Kimulwo alisema matokeo ya uchunguzi ya awali yanaonyesha marehemu alionekana kunyongwa na jicho moja lilitolewa nje.

Kimulwo alisema chifu aliarifu polisi kwamba sanduku la chuma lilidondoshwa kando ya barabara eneo la Kipkaren mnamo Januari 3 2023.

Wakaazi walipata maiti ya mtu mzima ikiwa imefungwa kwa vazi la mwanamke kwenye sanduku la chuma.