Serikali kuyafunga mashirika yote yasiyoleta faida

Mudavadi alisema serikali inanuia kuuza Mashirika ambayo yamekuwa mzigo kwa walipa ushuru.

Muhtasari

• Ripoti ya Uwekezaji wa Serikali ya Kitaifa mwaka wa fedha wa 2019-2020 ilionyesha kuwa kati ya mashirika 247 ya Serikali, 127 yalipata hasara.

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023 Picha: ANDREW KASUKU
Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi akihutubia wanahabari mjini Nairobi mnamo 19/01/2023 Picha: ANDREW KASUKU

Serikali itafunga mashirika yote ya umma yasiyo na faida, Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi amesema. 

Mudavadi alisema serikali inanuia kuuza Mashirika ya Serikali ambayo yamekuwa mzigo kwa walipa ushuru. 

"Hatujafanya vyema katika urekebishaji wa mashirika ya umma," Mudavadi alisema. 

Akihutubia wanahabari katika afisi yake jijini Nairobi, Mudavadi aliongeza kuwa baadhi ya mashirika ya Serikali huenda yakalazimika kufungwa kwa sababu yanategemea kabisa ufadhili wa serikali kwa shughuli zao.

 "Itatubidi kuamua ni mashirika gani ya Serikali yanayohalalisha uwepo wao. Maamuzi magumu yapo njiani,” alisema. 

Mashirika ya Serikali yasiyo na faida husababisha changamoto kubwa za kifedha kwa serikali kutokana na madeni yao makubwa na gharama zisizo endelevu. 

Kwa miaka mingi, utendaji wa kifedha na ufanisi wa uendeshaji wa mashirika mengi ya Serikali yamekuwa yakidorora, yakifyonza sana fedha za umma kwa kutegemea zaidi usaidizi wa kibajeti kutoka kwa Hazina ya Kitaifa. 

Mwaka 2021, ni mashirika machache ya Serikali yaliyopata faida. Mashirika hayo ni pamoja na Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), Kampuni ya Kenya Pipeline Ltd, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Kenya. 

Mashirika hayo hulipa ruzuku na kodi mara kwa mara na ndio yanayotoa kodi za juu zaidi miongoni mwa mashirika yanayomilikiwa na Serikali. Ingawa mashirika ya serikali si, na hayapaswi kuwa, makampuni ya kutengeneza faida lakini yanatarajiwa kuwa na salio mwishoni mwa mwaka wa fedha. 

Kusajili faida kwa shirika la Serikali huwa ishara ya matumizi bora ya fedha za umma. Mwaka 2020, ripoti ya Hazina ya Kitaifa iliyowasilishwa kwenye Bunge la Kitaifa ilionyesha kuwa zaidi ya nusu ya mashirika ya umma yamesajili hasara au na yanakabiliwa na matatizo ya kifedha. 

Ripoti ya Uwekezaji wa Serikali ya Kitaifa kwa mwaka wa fedha wa 2019-2020 ilionyesha kuwa kati ya mashirika 247 ya Serikali, 127 yalipata hasara. Shirika la Reli la Kenya (KRC), ambalo lilipata hasara kubwa zaidi katika kipindi hicho, hasara yake ilikaribia mara tatu kutoka Shilingi bilioni 8.47 mwaka wa 2019 hadi bilioni 24.2 mwaka jana. 

Kampuni zingine za Serikali ambazo hazikufanya vyema katika kipindi hicho ni pamoja na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) na Nzoia Sugar iliyopata hasara ya Shilingi bilioni 3.48.