Mwanamume aliyemchinja nyanyake kufanyiwa uchunguzi wa kiakili

Mshukiwa huyo alionekana kutoguswa alipofika kortini, pia inadaiwa kuwa awali alimuua jamaa mwingine.

Muhtasari
  • Waliokuwepo walidai mshukiwa alitaka pesa kutoka kwa mwanamke huyo mzee na alipokataa, mwanamume huyo alienda kumvamia

Mahakama imeamuru kufanyiwa uchunguzi wa kiakili Abdulaziz Swaleh, 20, ambaye anadaiwa kumchinja nyanyake eneo la Mji wa Kale, Mombasa.

Hakimu mkuu Vincent Adet pia aliwapa polisi muda zaidi kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.

Mshukiwa huyo alionekana kutoguswa alipofika kortini, pia inadaiwa kuwa awali alimuua jamaa mwingine.

Mwili wa Shariffa Ali Salim, 80, ulipatikana ukiwa umetapakaa kwenye dimbwi la damu nyumbani kwake Jumapili usiku muda mfupi baada ya tukio hilo.

Familia hiyo ilisema kuwa Swaleh alizozana na nyanyake ndani ya nyumba hiyo kabla ya kuchukua kisu cha jikoni na kukitumia kumkata shingo.

Waliokuwepo walidai mshukiwa alitaka pesa kutoka kwa mama huyo mzee na alipokataa, mwanamume huyo alienda kumvamia.

Msaidizi wa nyumbani ambaye alikuwa ndani ya nyumba alijaribu kumwokoa bila mafanikio.

Polisi walisema waliitwa kwenye eneo la tukio baada ya mshukiwa kukamatwa na wananchi alipokuwa akijaribu kutoroka.

Policw walipata walipata silaha ya muuaji kutoka eneo la tukio kabla ya kuupeleka mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti kusubiri uchunguzi wa maiti na uchunguzi zaidi.

Kesi hiyo itatajwa Februari 8.