IG Koome akiri kubadilishwa kwa walinzi wa Uhuru

IG alisema mabadiliko hayo hayana kinyongo na si ya kulipiza kisasi bali ni kuambatana na sheria za nchi.

Muhtasari

• Mkuu huyo wa polisi pia alithibitisha mabadiliko makubwa katika ulinzi wa waliokuwa mawaziri chini ya serikali ya Uhuru Kenyatta.

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome
Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome
Image: HISANI

Inspekta mkuu wa polisi Japhet Koome amekiri kubadilishwa kwa walinzi wa rais mustaafu Uhuru Kenyatta.

Akizungumza siku ya Ijumaa, Koome hata hivyo alipuuzilia mbali madai kwamba ulinzi wa rais Mustaafu Uhuru Kenyatta ulikuwa umeondolewa.

IG alisema mabadiliko hayo hayana kinyongo na si ya kulipiza kisasi bali ni kuambatana na sheria za nchi.

Alieleza kuwa kulingana na sheria afisa mkuu wa ulinzi wa rais Mustaafu anafaa kuwa wa cheo cha chini na sio naibu inspekta wa polisi ili pawepo utaribu mwafaka katika kutoa maagizo ya kazi.

“Ni ukweli afisa mkuu wa ulinzi wa rais mustaafu aliondolewa ili kupewa majukumu mengine yanayoambatana na cheo chake, afisa mwingine mwenye cheo cha chini tayari ametumwa kuongoza kikosi cha ulinzi wa rais mustaafu.”

Koome vile vile alikiri kuwa usalama wa Uhuru ulipunguzwa ili kuambatana na hadhi yake ya sasa kama rais mustaafu.

Aliwaeleza wakenya kuwa kamwe usalama wa Uhuru hauwezi kuondolewa kwani ni haki yake kama rais mustaafu kupewa ulinzi na serikali.

Alithibitisha kuwa bado familia na makazi ya waliokuwa maraisi bado zinapewa ulinzi wa kutosha.

Mkuu huyo wa polisi pia alithibitisha mabadiliko makubwa katika ulinzi wa waliokuwa mawaziri chini ya serikali ya Uhuru Kenyatta. Alisema kuwa walipunguza ulinzi wa maafisa hao ili kuiana na majukumu yao.

“Wengi mmesikia wakisema kwamba wamestaafu. Mara mimi siku hizi niko tu nyumbani siendi mahali, je unataka sasa maafisa kama hao wapewe ulinzi sawa na waziri wangu ambaye hata sasa hii yuko kazini.” Koome alisema.

Aliongeza kuwa idara ya polisi ni ile inayowajibika na hawawezi kufanya jambo kinyume cha sheria.

Koome alikariri msimamo wake wa kufanya kazi bila mapendeleo.

Kulikuwa na ripoti siku ya Alhamisi kuwa usalama wa rais mustaafu na famiia yake ulikuwa imeondolewa hatua ambayo ilionekana kuwakera watu wengi.