Machogu aamuru kurejeshwa kazini kwa VC wa chuo cha Meru baada ya wanafunzi kuandamana

Machogu alitaja hatua ya kusimamishwa kazi kwa Odhiambo kama isiyoeleweka.

Muhtasari

•Machogu ameamuru kurejeshwa kazini kwa VC Romanus Odhiambo wa Chuo Kikuu cha Meru ambaye alifurushwa.

Wanafunzi wa Meru University waandamana kufuatia kufurushwa kwa VC Odhiambo.
Image: HISANI

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ameamuru kurejeshwa kazini kwa VC Romanus Odhiambo wa Chuo Kikuu cha Meru ambaye alifurushwa.

Katika taarifa yake ya Jumatatu, Machogu alitaja hatua ya kusimamishwa kazi kwa Odhiambo kama isiyoeleweka.

Hatua hiyo pia ilisababisha wanafunzi kufanya maandamano yaliyopelekea shule hiyo kufungwa Jumatatu.

"Wizara inaagiza baraza la chuo kikuu kubatilisha uamuzi wa kumtuma Odhiambo likizo ya mwisho na kumteua kaimu VC," Machogu alisema.

"Baraza la chuo kikuu limeagizwa kuwezesha kurejeshwa kwa Odhiambo kama VC mara moja, kwa vyovyote vile kabla ya kufungwa kwa biashara mnamo Machi 7."

Baraza lilisema halijashawishika kuwa VC huyo wa zamani alistahili muhula wa pili.

“Baraza la chuo kikuu katika kikao chake kilichofanyika Februari 27, 2023, lilitathmini utendaji wako na kubaini kuwa ulikuwa chini ya matarajio. Kwa hivyo, baraza lilikataa kufanya upya kandarasi yako kama ilivyoombwa katika barua yako ya tarehe 20 Desemba 2022,” mwenyekiti Prof Bosire Mwebi alisema katika barua ya Februari 27, 2023.

Siku ya Jumatatu wanafunzi walidai uamuzi wa baraza la chuo kikuu ulichochewa kisiasa na walitaka VC arejeshwe kazini mara moja.

Rais wa muungano wa wanafunzi Kariuki Wachira, akiungwa mkono na mtangulizi wake Hunnington Oguk, aliwaongoza wanafunzi katika maandamano na kuwashirikisha polisi katika mbio Jumatatu asubuhi.