Ni wetu tayari! Gachagua amkaribisha mbunge Jalang'o wa ODM katika UDA

Gachagua pia alimtaka mbunge wa Daragoretti Kaskazini Beatrice Elachi kujiunga na Kenya Kwanza.

Muhtasari

• DP Gachagua alisimulia jinsi Jalang'o alivyofukuzwa wakati wa mkutano wa wabunge wa Azimio (PG).

•Wanachama wa chama cha ODM wamesema kuwa mkutano uliofanyika Ikulu ulikuwa wa manufaa ya kibinafsi.

akiwa na Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi gachagua jijini Nairobi mnamo Machi 6, 2023.
Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor akiwa na Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi gachagua jijini Nairobi mnamo Machi 6, 2023.
Image: PCS

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza hadharani kuwa mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o ni wa kambi ya UDA.

Akizungumza wakati wa uwekaji msingi wa mradi wa Starehe Affordable Housing, Gachagua alisimulia jinsi Jalang'o alivyofukuzwa wakati wa mkutano wa wabunge wa Azimio (PG).

"Huyu Jalang'o ni wetu, baada ya kukutana na rais wetu William Ruto kule State House kwa mambo ya maendeleo, alifukuzwa mkutanoni," alisema.

Gachagua pia alimtaka mbunge wa Daragoretti Kaskazini Beatrice Elachi kujiunga na kambi ya Kenya Kwanza kwani inaangazia maendeleo pekee.

“Nimefurahi sana kumuona Beatrice Elachi, tunataka uwe pamoja nasi, nikikuona kwenye maandamano nitasikitika, tunajua hujui kurusha mawe,” alisema.

Mwezi uliopita, Jalang'o alisema walinzi wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga walimwambia atoke nje muda mfupi baada ya kiongozi huyo wa ODM kuwasili kwa mkutano uliofanyika Machakos.

"Nilikuja hapa kwa sababu mimi ni mwanachama wa ODM na Azimio. Tulipoingia ndani kulikuwa na kundi la wavulana ambao walinizuia na kusema kwamba sitaingia," alisema kisha.

"Baba alipoingia, mlinzi wake mmoja aliniambia nitoke nje nami nikatoka nje."

Wanachama wa chama cha ODM wamesema kuwa mkutano uliofanyika Ikulu ulikuwa wa manufaa ya kibinafsi.

Mkurugenzi wa chama cha mawasiliano Philip Etale alitaja mikutano ya Ikulu kama mbinu ya kugeuza mawazo ya taifa kutoka kwa gharama ya juu ya maisha, ada za shule zisizostahimilika kwa watoto wao na ufisadi.

“Chama kimekuwa kikifuatilia kwa karibu shughuli za nyuma ya pazia zinazohusisha baadhi yao na leo ndiyo ilikuwa kilele,” alisema.