Maandamano katika ikulu kupinga gharama ya maisha

Waandamanaji wamekerwa na mageuzi mbalimbali yaliyoanzishwa na Rais William Ruto.

Muhtasari

• Polisi waliwekwa katika sehemu mbalimbali kwenye barabara kuu zikiwemo Barabara ya State House, State House Avenue, Processional Way na Dennis Pritt.

Usalama umeimarishwa karibu na Ikulu Picha: CYRUS OMBATI
Usalama umeimarishwa karibu na Ikulu Picha: CYRUS OMBATI

Maafisa kadhaa wa polisi waliojihami siku ya Jumatano waliweka vizuizi kwenye barabara zinazoelekea Ikulu ya rais mjini Nairobi kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanywa na baadhi ya Wakenya kuhusu gharama ya juu ya maisha.

Waandamanaji hao pia wamekerwa na mageuzi mbalimbali yaliyoanzishwa na Rais William Ruto.

Polisi waliwekwa katika sehemu mbalimbali kwenye barabara kuu zikiwemo Barabara ya State House, State House Avenue, Processional Way na Dennis Pritt ambapo walisimamisha kwa muda na kuwahoji madereva.

Maafisa hao walisema walikuwa chini ya maagizo kutowaruhusu waendesha pikipiki kwani wanaweza kutumika kuvusha umati hadi Ikulu kwa maandamano hayo.

Hatua hii inajiri wakati kuna hali ya mkanganyiko wa iwapo maandamano yaliyopangwa kufanywa na viongozi wa Azimio la Umoja yataendelea.

Makataa ya siku 14 yaliyotolewa na viongozi wa Azimio yanakamilika Jumatano na kumekuwa na mikutano ya kupanga mikakati ya maandamano hayo, maafisa walisema.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alimkumbusha Rais William Ruto kwamba ana hadi Jumatano usiku wa manane kujibu malalamishi yao, ambayo yalitolewa katika bustani ya Jeevanjee jijini Nairobi.

Akizungumza siku ya Jumanne, Raila alisema kuwa kwa kushindwa kuheshimu matakwa hayo, Azimio itaendelea na maandamano makubwa siku ya Alhamisi.

"Tunawataka msubiri, mwisho ni kesho (Jumatano) saa sita usiku. Kwa hiyo mtatusikia Alhamisi," alisema.

Raila mnamo Februari 22, aliupa utawala wa Ruto makataa ya siku 14 kushughulikia changamoto zinazowakabili wakenya kuhusu gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa haki katika uchaguzi, na ugawaji wa kazi za serikali.

Raila alikuwa amewataka wafuasi wake kusimama kidete akisema baada ya muda wake kumalizika, maandamano mitaani yataanza iwapo Ruto atashindwa kutii matakwa hayo.