Mwili wa mwanamume aliyetoweka wapatikana kwenye tanki katika kanisa, Moyale

Polisi wanasema hawajajua jinsi Duba alikufa lakini wanashuku kuwa ni kisa cha mauaji.

Muhtasari

•Wako Denge Duba, 25, alikuwa ametoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kugunduliwa kwenye tanki la maji taka mnamo Jumapili, Machi 5.

•Mkuu wa polisi wa eneo la Mashariki Rono Bunei alisema wanachunguza tukio hilo.

crime scene
crime scene

Polisi wanafanya uchunguzi baada ya mwili wa mwanamume kupatikana kwenye tanki la maji taka katika boma la kanisa la katoliki la Bori mjini Moyale.

Wako Denge Duba, 25, alikuwa ametoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kugunduliwa kwenye tanki la maji taka mnamo Jumapili, Machi 5.

Polisi wanasema bado hawajajua jinsi Duba alikufa lakini wanashuku kuwa ni kisa cha mauaji.

Tanki lina kina cha futi sita. Waumini wa kanisa hilo walisema kulikuwa na harufu mbaya na walipochunguza, waligundua mwili uliokuwa ukioza.

Polisi wanaoshughulikia suala hilo walisema walipeleka mwili huo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kusubiri uchunguzi wa maiti.

Mkuu wa polisi wa eneo la Mashariki Rono Bunei alisema wanachunguza tukio hilo.

Wakati huo huo, polisi wanachunguza kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 29 ambaye mwili wake ulipatikana katika nyumba yake eneo la Santac kando ya Barabara ya Ngong', Nairobi.

Mwili wa Mary Mwikali ulipatikana Jumatatu na mfanyakazi wake ambaye alikuwa ameripoti kuwa hapokei simu zake.

Nyumba ambayo mwili huo uligunduliwa ilikuwa imefungwa kwa ndani na iliwalazimu polisi na majirani kuingia ndani ili kuufikia mwili huo.

Mwili huo ulipatikana katika hali ya kawaida na ulionekana kuwa hapo kwa zaidi ya siku mbili.

Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema bado hawajajua chanzo cha kifo hicho.

Alisema mwili huo haukuwa na majeraha na kwamba wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa kifo hicho ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

Katika eneo la Kasarani, mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 42 ulipatikana katika nyumba yake.

Polisi walimtaja mtu huyo kuwa ni Robinson Mwaniki.

Mkewe alifika nyumbani siku ya Jumatatu na kumpata mwanamume huyo akiwa amelala kitandani akiwa na kitu cheupe mdomoni.

Polisi walisema bado hawajajua sababu ya kifo hicho na wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa maiti kueleza zaidi kuhusu kifo hicho.

Utafsiri: Samuel Maina