Moses Kuria, Isaac Ruto wavunja vyama na kujiunga na UDA ya Ruto

Wengine ni chama cha Umoja na Maendeleo kinachoongozwa na aliyekuwa gavana wa Embu Martin Wambora

Muhtasari
  • Malala alisema kuwa sita hao sasa watakuwa wanachama rasmi wa "familia ya UDA" na watashiriki katika shughuli zote za chama.
Moses Kuria, Isaac Ruto wavunja vyama na kujiunga na UDA ya Ruto
Image: TWITTER

Jumla ya vyama sita vimejiunga na United Democratic Alliance (UDA), Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala ametangaza.

Katika taarifa yake kwa vyumba vya habari Jumanne, Malala alisema kuwa sita hao sasa watakuwa wanachama rasmi wa "familia ya UDA" na watashiriki katika shughuli zote za chama.

Vyama hivyo vinaongozwa na Chama Cha Kazi (CCK), anayefahamika kuongozwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri la Biashara (CS) Moses Kuria na Chama Cha Mashinani (CCM) kinachoongozwa na Isaac Ruto.

Wengine ni chama cha Umoja na Maendeleo kinachoongozwa na aliyekuwa gavana wa Embu Martin Wambora, National Agenda Party of Kenya (Alfayo Agufana), Farmers Party (Irungu Nyakera) na Economic Freedom Party (Issack Hassan Abey).

Aidha Malala aliwataka viongozi wa chama hicho kuwasisitizia wanachama wao ili kutekeleza majukumu yao ya dhati katika kukijenga chama.

Pia aliwapongeza kwa kufanya “uamuzi usio na ubinafsi” akiwahakikishia kuwa wamefanya uamuzi wa kiungwana.

"Ndugu zangu, hamtajutia uamuzi huu wa ujasiri," alisema.

Muda mfupi baada ya Uchaguzi Mkuu, Moses Kuria alitangaza kuvunjwa kwa chama chake cha CCK mnamo Oktoba 2022, akibainisha kuwa tayari alikuwa amearifu Ofisi ya Msajili wa vyama vya kisiasa (ORRP) kuhusu kuhama kwake.