Wabunge wamtaka Ukur Yatani na Joseph Kinyua kufika mbele yao kuhojiwa

Iwapo atajitokeza, Yatani atakuwa Waziri wa kwanza kutoka utawala wa zamani kujibu maswali

Muhtasari
  • Ilidaiwa kuwa maafisa wakuu wa serikali katika utawala wa zamani walisimamia shughuli ya Ksh6 bilioni siku nne kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022
Waziri wa Fedha Ukur Yatani

Wabunge mnamo Alhamisi, Machi 16, walimtaka aliyekuwa waziri wa Hazina Ukur Yatani kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa  kuhusu sakata ya Ksh6 bilioni ya ununuzi wa Telkom.

Wanachama wa Kamati ya Idara ya Fedha walifanya uamuzi huo katika juhudi zao za kubaini uhalali wa mikataba iliyofanywa katika kashfa inayodaiwa kuwahusisha maafisa katika utawala wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

Aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua pia aliitwa na kamati hiyo kujibu maswali kuhusu unyakuzi huo huo.

Suala hilo liliibuka baada ya wabunge kukataa kuidhinisha mgao wa bajeti ili kulipia ununuzi wa hisa hizo kutokana na kukosekana kwa uwazi.

Ilidaiwa kuwa maafisa wakuu wa serikali katika utawala wa zamani walisimamia shughuli ya Ksh6 bilioni siku nne kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 bila kutafuta uhalalishaji kutoka kwa afisi husika.

Baadaye, Kamati ya Fedha chini ya uongozi wa Mbunge wa Molo Kuria Kimani ilijitolea kuchunguza mchakato uliofuatwa katika uondoaji na malipo ya Ksh6 bilioni mwanzoni mwa kipindi cha uchaguzi.

Iwapo atajitokeza, Yatani atakuwa Waziri wa kwanza kutoka utawala wa zamani kujibu maswali yanayohusiana na maamuzi yaliyofanywa wakati wa uongozi wao.

Hata hivyo wajumbe wa kamati hiyo walikariri kuwa wito huo haukumfungulia mashtaka afisa yeyote kati ya waliotajwa bali ni jitihada za kutoa mwanga juu ya shughuli hizo.