Hatutahudhuria maandamano ya Azimio-Wabunge wa ODM waliokutana na Ruto wakata kauli

Wabunge hao walisema kwamba wanatambua haki ya kila raia au kikundi cha raia

Muhtasari
  • Kulingana na wabunge hao, changamoto za sasa za kiuchumi zinazokabili Kenya hazitatatuliwa kwa makabiliano ya kisiasa

Wabunge tisa wanaodhaniwa kuwa waasi wa Orange Democratic Movement (ODM) wamewataka wapiga kura wao kukemea hatua ya Jumatatu iliyoitishwa na kiongozi wa chama chao Raila Odinga akisema hawatahudhuria. 

Kulingana na wabunge hao, changamoto za sasa za kiuchumi zinazokabili Kenya hazitatatuliwa kwa makabiliano ya kisiasa na aina nyinginezo za ushabiki wa kisiasa.

Wakihutubia mkutano na waandishi wa habari katika majengo ya Bunge siku ya Ijumaa, wabunge hao walisema ni wakati wa kuwa na mazungumzo ya kitaifa ya kiuchumi ili kutafuta suluhu la changamoto za pamoja za kiuchumi nchini.

“Acha ushindani wetu wa kisiasa uwe katika kiwango cha kushindana kwa mawazo ya kiuchumi. Kwa hivyo tunataka kuwahimiza Wakenya wote wanaotaka kushiriki katika maandamano yaliyopangwa kufanyika wiki ijayo, wafanye hivyo kwa amani na kwa njia ambayo itaimarisha utawala wa kidemokrasia na kutohimiza machafuko na kuvunja sheria na utulivu,” Wabunge hao walisema.

Aliandamana na Seneta wa Kisumu Prof Tom Ojienda na wabunge Gideon Ochanda (Bondo), Mark Nyamita (Uriri), Paul Abuor (Rongo), Elisha Odhiambo (Gem) na Felix Odiwour almaarufu Jalang’o (Langata).

Wabunge hao walisema kwamba wanatambua haki ya kila raia au kikundi cha raia kupiga na kufanya maandamano kama kielelezo cha matakwa yao ya kisiasa, hata hivyo wakisema kwamba vitendo hivyo lazima vifanywe kwa kuzingatia mipaka ya Katiba.