Waislamu mjini Eldoret waandamana barabarani kupinga LGBTQ

Waliongozwa na Mwenyekiti wa Maimamu katika eneo hilo Abubakar Bini na Imam Abdiaziz Muhammed.

Muhtasari
  • Waliongozwa na Mwenyekiti wa Maimamu katika eneo hilo Abubakar Bini na Imam Abdiaziz Muhammed.
Waislamu mjini Eldoret waandamana barabarani kupinga LGBTQ
Image: MATHEWS NDANYI

Waislamu mjini Eldoret wamefanya maandamano mitaani kupinga uamuzi wa hivi majuzi wa Mahakama ya Juu kuruhusu usajili wa mashirika ya LGBTQ.

Waislamu hao walimiminika mitaani wakiwa na mabango yenye maandishi kupinga uamuzi wa mahakama walioutaja kama jaribio la kuhalalisha mashirika ya LGBTQ.

Waliongozwa na Mwenyekiti wa Maimamu katika eneo hilo Abubakar Bini na Imam Abdiaziz Muhammed.

"Tunapinga kabisa majaribio yoyote ya kuanzisha tabia hiyo nchini. Huo ni utovu wa maadili na unakwenda kinyume na utamaduni na mila zetu", alisema Bini.

Alisema Bibilia na Kurani zote mbili ni wazi dhidi ya kitu chochote cha kufanya na LGBTQ au aina zingine zozote za uasherati.

Bini alisema wanataka kuchunguzwa upya uamuzi wa mahakama na kumtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kuhakikisha uamuzi huo umeondolewa katika mfumo wa mahakama.

Bini aliwakosoa majaji hao kwa kwenda kinyume na matakwa ya Wakenya na kupuuza mila na desturi za nchi.

Bini alisema wanaunga mkono kikamilifu mswada uliopelekwa bungeni na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali kusitisha aina yoyote ya mijadala kuhusu LGBTQ.

Imam Abdiaziz alisema watazidisha maandamano hayo hadi matakwa yao yataheshimiwa na serikali na mahakama.