Sudi kumsomesha urubani mvulana aliyegurumisha ndege na kuigongesha kwenye uzio Gilgil

Mbunge Sudi ametaka kijana huyo kutokamatwa na kusamehewa .

Muhtasari

•Mvulana huyo aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi siku ya Ijumaa baada ya kushindwa kuirukisha hewani ndege hiyo ya mmiliki shamba jirani.

•Sudi ameahidi kumpeleka kijana huyo katika shule ya urubani ili apate kufunzwa jinsi ya kuendesha ndege.

amejitolea kumsomesha urubani kijana aliyesababisha ajali ya ndege Gilgil
Mbunge Oscar Sudi amejitolea kumsomesha urubani kijana aliyesababisha ajali ya ndege Gilgil
Image: HISANI

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amewasihi maafisa wa polisi kutomzuilia mvulana wa miaka 17 ambaye alijaribu kuendesha ndege nyepesi katika eneo la Gilgil, kaunti ya Nakuru kabla ya kuigongesha kwenye uzio wa stima.

Mvulana huyo aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi siku ya Ijumaa baada ya kushindwa kuirukisha hewani ndege hiyo ya mmiliki shamba jirani.

Sudi hata hivyo amewataka maafisa wanaomzuilia kijana huyo mwenye shauku ya kuendesha ndege kumsamehe huku akiahidi kumpeleka katika shule ya urubani ili apate kufunzwa jinsi ya kuendesha ndege.

"Ninaomba mamlaka wamsamehe kijana huyu kutoka Gilgil. Msimkamate. Tafadhali mkabidhi kwangu, nitampeleka shule ya urubani," Sudi alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Baadhi ya wanamitandao akiwemo MCA wa Kileleleshwa Robert Alai walimpongeza mbunge huyo wa Kapseret na kuunga mkono kauli yake.

"Nakubali. Anafaa kusamehewa," Alai alisema.

Mvulana huyo alikamatwa siku ya Ijumaa baada ya kuingia kwenye gereji ya ndege katika shamba la kibinafsi katika eneo la Gilgil na kuwasha ndege nyepesi kabla ya kuigongesha kwenye uzio.

Nambari ya usajili ya ndege 5Y-AZA aina ya PA25 ni ya Peter White, ambaye ni mmiliki wa shamba.

White aliwaambia polisi kuwa alikuwa karibu na eneo la Ndume na baadaye akapata habari kwamba kijana huyo  anayetoka eneo hilohilo aliingia kinyemela kwenye shamba hilo na kuenda kwa gereji ya ndege hiyo iliyokuwa imeegeshwa pale.

Maafisa katika kituo cha polisi cha Gilgil walisema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa tatu unusu asubuhi, takriban kilomita 3 kusini mashariki mwa kituo hicho.

"Aligonga ukingo wa uzio na injini ya ndege ikazima na athari ikaifanya kusonga. Propela na upinde wa mbele uliharibika. Mshukiwa alitoka bila majeraha na yuko chini ya ulinzi wa polisi kusaidia uchunguzi," ripoti hiyo ilisema.

Mtoto huyo baadaye aliwaambia polisi kwamba ana shauku ya kuendesha ndege na alikuwa amejifunza mengi kuhusu ndege kutokana na kukaa kwake katika shamba la White.

Alisema alianzisha ndege na kuanza kusonga kwenye barabara lakini ilishindwa kupaa.

Ndege hiyo ilisogea umbali mfupi kabla ya kufika kwenye ukingo wa uzio ulio na stima, ikazima na kukwama.

Kelele ilipigwa na kijana huyo alikamatwa kabla ya polisi kuitwa kumchukua.

Ndege hiyo ilivutwa hadi kwenye gereji yake ambapo wataalam wataichunguza kwa matengenezo.