Wanafunzi 124 wa shule ya upili ya Mukumu Girls waugua kuhara

Daktari alisema kuwa wanafunzi zaidi wanaendelea kupokelewa katika hospitali hiyo.

Muhtasari

•Vipimo vya awali vilivyofanywa na maafisa wa afya ya umma vilitupilia mbali ugonjwa wa Kipindupindu.

•Maafisa hao walisema kuwa ulaji wa chakula kilichoathirika inaweza kuwa sababu ya wanafunzi hao kuhara.

Image: HISANI

Takriban wanafunzi 124 wa Shule ya wasichana ya Sacred Hearts Mukumu katika kaunti ya Kakamega wamelazwa katika hospitali ya Kakamega County General.

Ingawa haijabainika mara moja kile ambacho kinawaathiri wanafunzi hao, vipimo vya awali vilivyofanywa na maafisa wa afya ya umma vilitupilia mbali ugonjwa wa Kipindupindu.

Maafisa hao walisema kuwa ulaji wa chakula kilichoathirika inaweza kuwa sababu ya wanafunzi hao kuhara.

Afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Kakamega, David Alila alisema kuwa wanafunzi zaidi wanaendelea kupokelewa katika hospitali hiyo.

"Bado hatujajua sababu halisi ya kuhara ni nini. Bado tunaendelea na vipimo,” alisema.

Alisema hospitali hiyo itatoa ripoti ya kina baada ya kukamilisha vipimo.

Juhudi za kupata maoni kutoka kwa mkuu wa shule Fridah Amwayi hazikufua dafu kwani hakujibu simu.