Ruto hajakutana na Raila wala kuzungumza naye - Ichung'wah aweka mambo wazi

Ichung'wa alithibitisha kuwa hakuna makubaliano ya 'handshake' katika maelewano ya sasa.

Muhtasari

•Ichung'wah alieleza kuwa mbinu ya ushirikiano wa pande mbili unazingatia sana maslahi ya nchi, zaidi ya ya masuala ya vyama.

•Mbunge huyo alishikilia kuwa wakati wa mazungumzo na upinzani,  wataangalia masilahi ya Wakenya zaidi ya yote.

akizungumza katika Kianyaga Boys Jumamosi.
Kiongozi wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wa akizungumza katika Kianyaga Boys Jumamosi.

Kiongozi wa wengi katika bunge Kimani Ichung'wah amesema Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga bado hawajakutana.

Ichung'wa alithibitisha kuwa hakuna kitu kinachohusu makubaliano ya 'handshake' katika maelewano ya sasa.

Akizungumza na vyombo vya habari siku ya Jumatatu, mbunge huyo wa eneo la Kikuyu alieleza kuwa mbinu ya ushirikiano wa pande mbili unazingatia sana maslahi ya nchi, zaidi ya ya masuala ya vyama.

"Naweza kuthibitisha kuwa Rais hata hajakutana na Raila Odinga, hata hajazungumza naye acha kupeana mkono," alisema.

Mbunge huyo alishikilia kuwa wakati wa mazungumzo na upinzani,  wataangalia masilahi ya Wakenya zaidi ya yote.

"Tunaangalia mkabala wa kuegemea pande mbili juu ya mkabala wa upendeleo ambao unaweza kuegemea upande mmoja au mwingine na hauhusiani kabisa na kupeana mkono," Ichung'wah alisisitiza.

"Naweza kukuthibitishia kwamba hakuna kupeana mikono."

Akihutubia taifa siku ya Jumapili, Rais Ruto alimtaka Raila kusitisha maandamano ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.

"Ninamsihi Raila na upinzani kusitisha maandamano na kutoa mbinu ya pande mbili ili tupeleke Kenya mbele," alisema.

Ruto hata hivyo alishikilia kuwa mazungumzo hayo lazima yazingatie mijadala ya dhati inayozingatia utawala wa sheria.

"Msimamo wetu ni kwamba tunataka kuwashirikisha ndugu na dada zetu kwa upande mwingine kuhusu masuala ambayo ni muhimu kwa Wakenya, wao kama upinzani, sisi kama serikali," alisema.

Akikaribisha wito huo, Raila alisema mchakato huo unapaswa kuanza “mapema kesho” (Jumatatu).

"Tuko tayari kushiriki na tutashiriki bila aina yoyote ya ufisadi na mchakato huu unapaswa kuanza mapema kesho," alisema Jumapili.

Hatua ya viongozi hao wawili imepongezwa na mataifa, mashirika na viongozi mbalimbali kote duniani.