Wakazi walipora mchele badala ya kuwaokoa waathiriwa wa ajali ya Migori -Polisi

Shehena nzima ya mchele, kiasi cha magunia 100 yalibebwa na wakazi.

Muhtasari

•Ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori kushindwa kulidhibiti na kuwagonga waendesha bodaboda katika mji wa Migori.

•"Polisi walilazimika kuwaokoa waathiriwa kwanza," Wanjala alisema.

Wananchi wakiwa kwenye shuguli ya uporaji baada ya ajali
Image: MANUEL ODENY

Polisi wamefichua kuwa wakaazi wa Migori walitangulia kupora mchele badala ya kuwaokoa waathiriwa wa ajali iliyosababisha vifo vya watu saba.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa mija asubuhi baada ya dereva wa lori kushindwa kulidhibiti na kuwagonga waendesha bodaboda katika mji wa Migori.

Lori hilo lilikuwa likisafirisha mchele kuelekea Isebania ajali hiyo ilipotokea.

Kamanda wa kaunti ya Migori Mark Wanjala alisema baada ya ajali hiyo, watu wa kwanza kufika katika eneo la tukio waliamua kupora mchele badala ya kutoa huduma ya kwanza kwa waathiriwa.

“Wakati wengine wakihitaji huduma ya kwanza, wananchi waliofika waliamua kuanza kwa kupora mchele kwenye lori, jambo ambalo linasikitisha,” alisema.

Chini ya muda mfupi, shehena nzima ya mchele, kiasi cha magunia 100 yalibebwa na wakazi.

"Polisi walilazimika kuwaokoa waathiriwa kwanza," Wanjala alisema.

Takriban watu kumi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Migori huku maafisa wa polisi wa trafiki wakielekeza msongamano wa magari kutoka mjini huku shughuli za uokoaji zikiendelea.

Polisi wanasema watatu wako katika hali mbaya.