Mwanaume ajitoa uhai kando ya barabara Mai Mahiu

Mwili wa marehemu ulipatikana ukining'inia kutoka kwa mti.

Muhtasari

•Mwili wa mwanamume huyo ambaye hakuwa na stakabadhi zozote za utambulisho ulipatikana ukining’inia kutoka kwa mti.

•Jaribio la kundi la vijana kuiba katika duka moja eneo la Ndabibi, Naivasha liliishia pabaya baada ya mmoja wao kuuawa.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Polisi katika eneo la Mai Mahiu, Naivasha wanachunguza kisa cha kustaajabisha ambapo mwanamume asiyejulikana alijitoa uhai kando ya barabara kwa kutumia kamba.

Mwili wa mwanamume huyo ambaye hakuwa na stakabadhi zozote za utambulisho ulipatikana ukining’inia kutoka kwa mti katika kituo cha biashara chenye shughuli nyingi.

Joel Kimani, mkazi wa eneo hilo alisema kuwa haijabainika iwapo mwanamume huyo aliyevalia nadhifu alijiua au maiti yake ililetwa katika eneo la tukio.

"Hakuna anayemjua mtu huyu na tunashangaa kwa nini alilazimika kusafiri kutoka popote alipotoka na kujiua hapa," alisema.

OCPD wa Naivasha Samuel Waweru alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa mwili huo ulikuwa umechukuliwa na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya eneo hilo.

"Maafisa wa uchunguzi wamekusanya alama za vidole kwa madhumuni ya utambuzi na faili ya uchunguzi imefunguliwa kama sehemu ya uchunguzi," alisema.

Huku hayo yakijiri, jaribio la kundi la vijana kuiba katika duka moja eneo la Ndabibi, Naivasha liliishia pabaya baada ya mmoja wao kuuawa kwa kuchomwa na mwingine kujeruhiwa vibaya na wananchi.

Wakati wa jaribio hilo la ujambazi lililoshindikana katika kituo kikuu cha biashara, kijana mwingine alitoroka na majeraha huku wakaazi wakilaani kuongezeka kwa visa vya uhalifu.

Shida ilianza baada ya vijana sita kuingia katika moja ya duka asubuhi ya Jumanne wakiwa na lengo la kubeba bidhaa.

Kulingana na Asef Kariuki, chifu, Ndabibi ya Kati, mmiliki huyo wa duka alikuwa amelala katika chumba kilicho karibu na alipopata ufahamu wa wizi huo na kuwaarifu majirani zake.

Aliongeza kuwa wakazi hao walifanikiwa kuwakamata watatu kati ya vijana hao na kumchoma mmoja wao huku polisi wakimuokoa wa pili na wa tatu akitumia giza kutoroka.

"Tunatoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi na kuwakabidhi watuhumiwa kwa polisi badala ya kuwaua," alisema.

Aliongeza kuwa polisi wameanzisha msako wa kuwasaka washukiwa hao akiwemo aliyekimbia na majeraha yaliyotokana na wananchi.