Wakenya wengi wanamtaka Uhuru kustaafu siasa -Kura ya Maoni

Asilimia 59 ya Wakenya wanamtaka rais mstaafu, Uhuru Kenyatta kujitenga kabisa na masuala ya siasa,

Muhtasari

•Asilimia 36 pekee ya Wakenya ndio wanataka kiongozi huyo wa taifa wa zamani aendelee kutoa mchango wake katika siasa za nchi.

•Utafiti huo ulifanyika kati ya Machi 11 hadi Machi 19, 2023 na ukingo wa makosa ni ± 2.12%.

Rais mstaafu akataa mwaliko wa kuongoza mazungumzo ya amani Ethiopia
Rais mstaafu akataa mwaliko wa kuongoza mazungumzo ya amani Ethiopia
Image: Maktaba

Takriban asilimia 59 ya Wakenya wanamtaka rais mstaafu, Uhuru Kenyatta kujitenga kabisa na masuala ya siasa za nchi na kufurahia ustaafu wake pamoja na familia yake, kura mpya ya maoni ya TIFA imebaini.

Kura hiyo ya maoni ambayo ilitolewa siku ya Alhamisi inaonyesha kwamba asilimia 36 pekee ya Wakenya ndio wanataka kiongozi huyo wa taifa wa zamani aendelee kutoa mchango wake katika siasa za nchi.

5% ya Wakenya hata hivyo hawana uhakika ikiwa wangetaka Uhuru aendelee kuunga mkono viongozi anaowakubali na sera anazokubaliana nazo ama anafaa kuangazia mambo mengine kama biashara za familia.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Machi 11 hadi Machi 19, 2023 na ukingo wa makosa ni ± 2.12%.

Miongoni mwa wafuasi wa Muungano wa Kenya Kwanza, asilimia 70 wanamtaka kiongozi huyo wa chama cha Jubilee ajiepushe kabisa na siasa huku asilimia  26 pekee wakitaka aendelee kujihusisha na siasa za nchi.

Asilimia 51 ya wafuasi wa Azimio la Umoja wangetaka rais huyo mstaafu aangazie mambo mengine bali na siasa huku 45% wakitaka aendelee.

Utafiti ulifanyika katika maeneo 9 ya nchi; Bonde la Ufa Kati, Pwani, Mashariki ya Chini, Mlima Kenya, Nairobi, Kaskazini, Nyanza, Ufa Kusini, na Magharibi. Katika maeneo ya Nyanza na Mashariki ya Chini, wengi wanataka rais huyo wa zamani aendelee kuhusika huku katika maeneo mingine 6, wengi wakitaka astaafu.