Mhubiri Paul Mackenzie kuepuka mashtaka ya mauaji ya halaiki

Mackenzie huenda akaepuka mashtaka ya mauaji ya halaiki

Muhtasari

• Waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki alitangaza msitu wa Shakahola kuwa eneo la uhalifu na kuamuru kwamba unapaswa kufungwa kabisa.

MCHUNGAJI: Mhubiri wa televisheni Paul Mackenzie akiwa mahakamani Malindi mnamo Alhamisi Machi 23. Picha: ALPHONCE GARI
MCHUNGAJI: Mhubiri wa televisheni Paul Mackenzie akiwa mahakamani Malindi mnamo Alhamisi Machi 23. Picha: ALPHONCE GARI

Mashtaka ya mauaji ya halaiki, ugaidi na uhalifu dhidi ya ubinadamu ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na DCI wanapanga kumfungulia Mchungaji Paul Mackenzie hayana mashiko, baadhi ya mawakili wa uhalifu wamesema.

Siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alipokuwa kwenye ziara ya ekari 800 katika msitu wa Shakahola, ambapo miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Mackenzie wamekuwa wakifukuliwa, alitaja vifo hivyo kuwa mauaji ya halaiki.

Kufikia Alhamisi, miili 95 ya watu waliokuwa wamezikwa kwa siri katika msitu huo mkubwa, ilikuwa imefukuliwa. Takriban wahasiriwa 37 walikuwa wameokolewa na kupelekwa hospitalini.

Kindiki, ambaye Jumapili alitangaza msitu wa Shakahola kuwa eneo la uhalifu na kuamuru kwamba unapaswa kufungwa kabisa, alisema DPP Noordin Haji na DCI Mohammed Amin, wanachunguza matukio hayo ili kumfungulia mashtaka kasisi Mackenzie kwa mauaji ya halaiki na mashtaka yanayohusiana na ugaidi.

"Hapo, kesi ya ugaidi inaweza kuwasilishwa ili kumshtaki Mackenzie na washirika wake. Wanaweza pia kushtakiwa kwa uhalifu wa mauaji ya halaiki chini ya sheria za Kenya na chini ya mkataba wa kimataifa,” alisema.

“Serikali itafanya kila iwezalo kumtia hatiani Mackenzie na wale wote waliomsaidia kufanya uhalifu huo. Wote watalipa, na usitegemee kuwa atakuwa nje ya jela maisha yake yote.”

Rais William Ruto pia amelinganisha matukio ya Shakahola na ugaidi.

"Tunachokiona Kilifi, Shakahola, ni sawa na ugaidi. Magaidi hutumia dini kuendeleza vitendo vyao viovu. Watu kama Mackenzie wanatumia dini kufanya maovu," Ruto alisema Jumatatu.

Hata hivyo, mawakili nchini wametathmini suala hilo wakisema mashtaka ya mauaji ya halaiki na ugaidi dhidi ya Mackenzie hayawezi kuthibitishwa katika mahakama yoyote.

Dkt Sarah Kinyanjui, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Mombasa, alisema vitendo vya Mackenzie ni vya kuchukiza na vikubwa, sio tu kwa kiasi bali pia katika hali ya kinyama ambayo vilitekelezwa. Hata hivyo, alisema changamoto kwa DPP itakuwa ni kusawazisha matakwa ya umma na mkakati wa kupata hatia kwa kuthibitisha mashtaka yake. 

"Uzito wa makosa unatoa matarajio ya umma ya mashtaka makubwa zaidi. Lakini, ili kupata hatia, DPP atalazimika kutafuta kosa kubwa zaidi ambalo linaweza kutoa hatia,” Kinyanjui alisema. 

Aliongeza; "Uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mfano ni shtaka kubwa, lakini kuafikia vigezo vya kisheria ili kufanikisha mashtaka ni kibarua kizito kwa DPP." 

Alisema uamuzi wa DPP pia utaongozwa na kuzingatia ushahidi.

 "Yote yatategemea ushahidi wanaoupata, ambao unaweza kuwa hauko hadharani kwa sasa," alisema. 

Benjamin Njoroge, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Mombasa, aliambia Star kuwa wazo la kumshtaki Mackenzie kwa mauaji ya halaiki na ugaidi halima mashiko. 

"Ningependa kumwambia DPP kuwa wabunifu sana kuhusu mashtaka ambayo yatashinikizwa kwa mchungaji huyo kwa sababu itakuwa vigumu kuthibitisha bila shaka kwamba mauaji ya halaiki yalifanyika," Njoroge alisema. 

Dkt Duncan Ojwang, mhadhiri wa sheria jijini Nairobi, alisema katika kesi ya mauaji ya halaiki, upande wa mashtaka unapaswa kudhibitisha kwamba kulikuwa na mauaji ya kimakusudi ya kikundi cha watu, kwa ujumla au kwa sehemu. 

"Lazima uthibitishe kuwa kulikuwa na nia ya kuharibu kabila, rangi, dini au kikundi chochote cha watu. Katika kisa cha Mackenzie, unathibitishaje kwamba kasisi alikuwa amekusudia kuangamiza kikundi hicho cha watu?” Ojwang alihoji. 

"Lazima uthibitishe kuwa Mackenzie alikuwa akiua kwa lengo la kuondoa kundi hilo." Kulingana na Dkt Ojwang, ambaye ni Mkuu wa zamani wa kitengo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha African Nazarene, kesi inayoweza kumhukumu Mackenzie ni pamoja na; utupaji haramu wa miili, kuvamia shamba la ekari 800 kinyume cha sheria (ikiwa hana hati za umiliki halali) na kuanzisha vituo kinyume cha sheria ya utaratibu wa umma. 

“Tunaweza kutaka kujua kwa nini miili hiyo ilikuwa inazikwa bila kutoa taarifa kwa mamlaka, hilo ni shtaka linaloweza kumtia hatiani Mackenzie. Baada ya hapo, atalazimika kuthibitisha kwamba hakuwahi kuhusika katika vifo vyao,” alisema.

Alisema si rahisi kuwasilisha mashtaka tu bila ukweli, kwa hivyo, DCI na DPP wanapaswa kuruhusu ukweli na ushahidi kuwaongoza kwenye mashtaka. Pia aliwataka DPP na DCI kuwafuata wahasiriwa wa Mackenzie na kuwashtaki kwa kujaribu kujiua au utelekezaji (kwa wale ambao watoto wao wamekufa). 

"Kwa wahasiriwa, ambao watoto wao wamekufa, itakuwa rahisi kuwatia hatiani kwa utelekezaji uliosababisha vifo vya watoto wao. Wanaweza pia kushtakiwa kwa kujaribu kujiua, na kwa hivyo, Mackenzie pia anaweza kushtakiwa kwa kusaidia uhalifu huo,” alisema. 

Paul Magolo, wakili wa uhalifu anayehudumu Mombasa, alisema Mackenzie anaweza kuondoka bila kukutwa na hatia yoyote kwa sababu mashtaka ya mauaji ya halaiki hayawezi kuthibitishwa dhidi yake. 

"Hatusemi kwamba hana hatia, lakini shtaka la mauaji ya halaiki ambalo linawekwa dhidi ya Mackenzie linaweza kuwa gumu kuthbitishwa," alisema. 

Wakati huo huo, Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya Eric Theuri, alisema wameunda kikosi cha mawakili ambao watasaidia DCI na DPP kumshtaki Mackenzie. 

"Kama LSK, hatuwezi kusema ni mashtaka gani yanafaa kufunguliwa dhidi ya mhubiri, lakini tumeunda timu ambayo itashirikiana na DPP na DCI kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata haki," Theuri alisema. 

Alisema LSK inataka kuangalia jinsi waathiriwa wa mafundisho ya Mchungaji Mackenzie watakavyofidiwa na wengine kurejeshwa makwao. 

"Tunataka waathiriwa ambao wamepoteza mali zao, wale ambao wamepoteza maisha yao, na wale ambao wamepoteza watoto wao, walipwe fidia ipasavyo na mchungaji huyo," alisema.