Ruto amteua Jaji Lessit kuongoza tume itakayochunguza mauaji ya Shakahola

Rais Ruto pia aliwateua Vivian Janet Nyambeki na Bahati Mwamuye kuwa mawakili wasaidizi wa tume hiyo.

Muhtasari
  • Timu inayoongozwa na Jaji Lessit pia itachunguza mazingira ambayo vifo hivyo vilitokea, na "kuchunguza makosa ya kisheria
JAJI JESSIE LESSIT
Image: HISANI

Rais William Ruto sasa ameunda Tume ya Uchunguzi inayojumuisha wanachama 13 kuanza uchunguzi kuhusu mauaji ya Shakahola ambapo zaidi ya watu 100 wameripotiwa kufariki kufikia sasa.

Rais Ruto, katika notisi ya gazeti la serikali iliyotolewa Ijumaa, alitaja wanachama 8 wa tume hiyo itakayoongozwa na Jaji Jessie Lessit.

Wajumbe wengine watakuwa; Lady Justice (Mst.) Mary Muhanji Kasango, Eric Gumbo, Askofu Catherine Mutua, Dkt. Jonathan Lodompui, Dkt. Frank Njenga, Wanyama Musiambu na Albert Musasia.

Rais Ruto pia aliwateua Vivian Janet Nyambeki na Bahati Mwamuye kuwa mawakili wasaidizi wa tume hiyo.

Mkuu wa nchi katika notisi hiyo, aliipa tume hiyo jukumu la kuchunguza vifo hivyo pamoja na madai ya kuteswa na kuwatendea kinyama wafuasi wa aliyejiita kasisi Paul Mackenzie na kanisa lake la Good News International lenye makao yake makuu katika Kaunti ya Kilifi.

Timu inayoongozwa na Jaji Lessit pia itachunguza mazingira ambayo vifo hivyo vilitokea, na "kuchunguza makosa ya kisheria, kitaasisi, kiutawala, kiusalama na ya kijasusi ambayo yanaweza kuwa yamechangia kutokea kwa mkasa wa Shakahola."

“Tambua, kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa mbele ya Tume, watu na asasi zinazobeba dhamana kubwa zaidi ya Msiba wa Shakahola, na kupendekeza hatua mahususi zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na mawaidha, hatua za udhibiti, malipo, au mapendekezo ya uchunguzi wa makosa ya jinai; ” alisema Rais.

Aidha aliongeza kuwa tume hiyo inapaswa; "Pendekeza hatua za kisheria, kiutawala, au aina nyingine za uwajibikaji dhidi ya afisa yeyote wa umma ambaye hatua au kutotenda kwake kunathibitishwa kuwa kumechangia kwa makusudi au kwa uzembe kutokea kwa Janga la Shakahola."