Wakili Kipkorir ajawa matumaini huku akimsafirisha mamake kwenda India kwa matibabu

"Mamangu Mpendwa Katarina amepitia maumivu makali sana .Naomba madaktari bora wa Kansa nchini India wampe utulivu na uponyaji," Kipkorir alisema.

Muhtasari

•Kipkorir alifichua kuhusu ziara hiyo yake kwenye Twitter na kuelezea matumaini yake makubwa kuwa mamake atapona.

•Wakili huyo alirejerea Biblia kuhusu amri ya kuwaheshimu wazazi, akibainisha kwamba amri hiyo ni hakikisho ya baraka.

akimsafirisha mamake kwenda India mnamo Mei 19,2023.
Wakili Donald Kipkorir akimsafirisha mamake kwenda India mnamo Mei 19,2023.
Image: TWITTER// DONALD KIPKORIR

Siku ya Ijumaa, Wakili mashuhuri Donald B. Kipkorir aliondoka nchini kuelekea India [pamoja na mama yake ambako mzazi huyo wake atafanyiwa matibabu.

Kipkorir alifichua kuhusu ziara hiyo yake kwenye Twitter na kuelezea matumaini yake makubwa kuwa mamake atapona.

Alisema walikuwa wakisafiri kwa ndege kwenda India kuonana na daktari wa saratani, na kuongeza kuwa mzazi huyo wake amepitia maumivu mengi katika safari yake ya ugonjwa.

“Niko njiani kuelekea India na mama yangu. Amri ya kuwaheshimu wazazi wetu ndiyo Amri pekee iliyo na Baraka za uhakika,” Kipkorir alisema Ijumaa.

Aliongeza, “Mama yangu Mpendwa Katarina amepitia maumivu makali sana .Naomba kwamba Madaktari Bora wa Kansa nchini India wampe utulivu na uponyaji. Mbingu na zitusikie.”

Wakili huyo aliambatanisha ujumbe huo wake na picha yake na mamake wakiwa ndani ya ndege.

Alirejerea Biblia kuhusu amri ya kuwaheshimu wazazi, akibainisha kwamba amri hiyo ni hakikisho ya baraka.

Waefeso 6:2-3 inasema: “Waheshimu baba yako na mama yako, ambayo ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, ili upate heri na uishi maisha marefu duniani.”

Mamake Donald B. Kipkorir amekuwa akiugua ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu.

Mwezi Septemba mwaka wa 2022, wakili huyo aliandika ujumbe wa dhati kwa mamake, akimtakia afueni ya haraka.

Wakati huo, alisema mama yake anakabiliana na maumivu baada ya vipindi vya matibabu ya radiotherapy na kuwataka wafuasi wake wamkumbuke katika maombi.

"Leo, sala na mawazo yangu ni kwa mama yangu ambaye anabeba maumivu, uchungu na madhara ya vipindi vya radiotherapy. Maombi yenu na yatikise mbingu ili kumponya mama yangu: maadili yangu na maisha ya North Star," alisema.

Sote tunamtakia mamake Kipkorir heri anapopata matibabu na tunaomba aweze kupata afueni ya haraka.