Jalang'o, Babu Owino miongoni mwa wabunge wanaokabiliwa na hatua za kinidhamu kuhusu mswada wa fedha

“Kwa hiyo Chama kimeanza taratibu za kinidhamu dhidi ya wanachama,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Muhtasari
  • Zaidi ya hayo, chama hicho pia kilidokeza kuwa kitachukua hatua za kinidhamu dhidi ya wabunge 24 ambao hawakuwepo
Jalang'o asema wanablogu ndio walijiingiza kwenye mtego na ameshindwa kuwatetea dhidi ya kutokatwa ushuru.
Jalang'o asema wanablogu ndio walijiingiza kwenye mtego na ameshindwa kuwatetea dhidi ya kutokatwa ushuru.
Image: Instagram

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) mnamo Alhamisi, Juni 15, kilianza hatua za kinidhamu dhidi ya Wabunge wanne waliounga mkono kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2023.

Watakaokabiliwa hatua za  kinidhamu ni pamoja na; Esther Passaris (Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi) na Elisha Ochieng Odhiambo (Mbunge wa Gem).

Wengine ni Aden Adow Mohamed (Mbunge wa Wajir Kusini) na Caroli Omondi (Mbunge wa Suba Kusini).

“Chama kinapokea malalamiko mengi kutoka kwa wanachama wake kwa ujumla kuhusu mienendo ya wajumbe wake wa Bunge wakati wa upigaji kura wa jana wa Muswada wa Sheria ya Fedha, 2023.

“Kwa hiyo Chama kimeanza taratibu za kinidhamu dhidi ya wanachama,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Zaidi ya hayo, chama hicho pia kilidokeza kuwa kitachukua hatua za kinidhamu dhidi ya wabunge 24 ambao hawakuwepo wakati wa mjadala wa Mswada wa Fedha wa 2023 mnamo Jumanne, Juni 14.

Baadhi ya wabunge waliokosekana wakati wa mjadala huo ni; Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, John Mbadi (aliyeteuliwa), Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor (Jalang’o) na Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda.

Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang na Mark Nyamita wa Uriri pia walijumuishwa kwenye orodha hiyo.

“Kwa kuzingatia kanuni za kinidhamu za chama, notisi za kuonyesha sababu kwa nini hatua za kinidhamu zisichukuliwe zimetolewa kwa wanachama hao.

"Wanatarajiwa kujibu ndani ya saa 48 zijazo," Katibu Mkuu Edwin Sifuna alielekeza.

Azimio la Umoja ilikuwa imeazimia kupinga Mswada wa Fedha wa 2023 kwa jumla kuhusu mapendekezo waliyoyataja kuwa ya juu ya kodi ikiwa ni pamoja na ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5.