ODM yawaanika wanachama ambao hawajajibu baada ya kukaidi msimamo wa chama

ODM ilifichua kuwa wanachama 17 wa chama hicho tayari wamejibu barua hiyo.

Muhtasari

•Chama hicho kiliwapa barua wanachama wake 30 ambao hawakufuata msimamo wa chama kuhusu mswada wa Fedha wa 2023.

•Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwour na mwenzake wa Rarienda Otiende Amollo ni miongoni mwa wanachama 13 ambao bado hawajatuma majibu yao

Raila Odinga
Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Image: TWITTER

Chama cha ODM kimetoa taarifa kuhusu majibu ya wanachama waliokaidi msimamo wa chama kuhusu Muswada wa Fedha wa 2023 wiki jana.

Wiki iliyopita, chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga kiliwapa barua wanachama wake 30 ambao hawakufuata msimamo wa chama kuhusu mswada huo tata baada ya kupitishwa kwake kwa kura nyingi.

Katika taarifa ya siku ya Jumanne, ODM ilifichua kuwa wanachama 17 wa chama hicho tayari wamejibu barua hiyo.

“Majibu yaliyopokelewa hadi sasa yanashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni ya Kamati ya Nidhamu (Matendo na Utaratibu) ya ODM, 2022 na wanachama husika watajulishwa uamuzi huo kwa wakati ufaao,” taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa chama hicho. Edwin Sifuna alisoma.

Miongoni mwa wanachama ambao wametuma majibu tayari ni John Mbadi, Eve Obara, Joyce Bensouda, Paul Abuor, Elisha Odhiambo, Adow Mohamed, Esther Passaris, Caroli Omondi, Babu Owino na George Aladwa.

Wengine ni Johnson Naicca, Kakuta MaiMai, Irene Mayaka, Peter Oscar Nabulindo, Christopher Aseka, Tindi Mwale na Samuel Parashina.

Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwour na mwenzake wa Rarienda Otiende Amollo ni miongoni mwa wanachama 13 ambao bado hawajatuma majibu yao. Wengine ni pamoja na Gideon Ochanda, Joseph Oyula, John Ariko Namoit, Paul Nabuin, Said Buya Hiribae, Mohamed Abdikadir Hussein, Titus Khamala, Wilberforce Oundo, Mark Nyamita, Daniel Manduku na Fatuma Masito.

"Pia tunachukua fursa hii kumwomba radhi Mhe Tom Kajwang ambaye jina lake liliingizwa kimakosa katika taarifa yetu ya tarehe 15 Juni 2023," taarifa hiyo ilisomeka.